PALIKUWA hapatoshi! Matukio matano yametikisa usiku wa kuamkia jana Ijumaa ndani ya Hoteli ya Best Western Coral Beach iliyopo Masaki jijini Dar baada ya kufanyika baby shower ya mama kijacho wa mfalme wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna raia wa Kenya. Pati hiyo ilihudhuriwa na watu kibao wakiwemo Jacqueline Wolper, Irene Uwoya na Shilole, Hadija Shaibu ‘Dida’, Asha Baraka na wengineo. Ukiweka pembeni masuala ya kula, kunywa na kujiachia kwa kucheza, yapo matukio matano yaliyotikisa.

MAMA D ‘KUMKUNIA NAZI’ ANKO SHAMTE

Mama wa Diamond Platnumz, Sanura Kassim ‘Mama D’ pamoja na mumewe, Anko Shamte waliingia kwa mbwembwe ukumbini hapo kama kawaida yao lakini walinogesha zaidi mbwembwe zao pale Mama D ‘alipomkunia nazi’ Anko Shamte wakati wakipiga picha za mapozi.

VERA SIDIKA ACHOMOA BETRI

Wakati Mashikolo Mageni wakishangaa hayo, mwanamuziki na mfanyabiashara kutoka Kenya, Vera Sidika alikuwa balaa au unaweza kusema alichomoa betri kwa maneno ya vijana wa kileo baada ya kuvamia eneo la tukio akiwa na kivazi kilichoacha wazi sehemu kubwa ya maungo yake hasa yale nyeti.

Vera alisababisha umati uliofurika eneo hilo kuvunja shingo kukodolea vizuri kivazi hicho kilichoonekana kuwamwaga udenda wanaume wakware lakini mwenyewe alionekana kutojali.

UWOYA, LAVALAVA FULL KUBEBISHANA

Msanii wa Bongo Muvi, Irene Uwoya na mwanamuziki wa WCB, Lavalava nao walikuwa gumzo kwenye pati hiyo kwa jinsi walivyokuwa wakibebishana na kusindikizana kila kona.

Licha ya Uwoya kuingia na gauni lililokuwa likimpa tabu kulishika mara kwa mara, alikuja kupata usaidizi wa Lavalava ambapo kuna wakati alionekana kama mpambe wa bi harusi kwa kulishika na kuonekana wakibembelezana.

DIAMOND ALALIA KITANDA CHA MTOTO

Wakati mambo yakiwa yamenoga kwenye pati hiyo, ulifika wakati wa kutoa zawadi ambapo Esma ambaye ni dada wa Diamond baada ya kumkabidhi Tanasha zawadi kibao ikiwemo kitanda cha mtoto anayetarajiwa kuzaliwa, msanii huyo ilikuwa ni kama anakionja baada ya kukilalia huku akijigaragaza kama yuko kwenye kitanda cha mtu mzima.

Jambo hilo lilionekana kama kituko, wengine wakisema hiyo ilisababishwa na furaha ya kufanya pati hiyo.

MGENI MUALIKWA AKAMULIWA NDIMU

Kunoga kwa pati hiyo kulisababishwa na mengi ambapo upande wa vinywaji ulikuwa siyo kwa staili ile ya ‘mupe muruke’ na ndipo mwanamke mmoja ambaye alifika na kampani ya Esma alipozimia kwa kilevi hivyo kubebwa na wafanyakazi wa hoteli mpaka sehemu maalum na kuanza kumka-mulia ndimu mdomoni na miguuni kama huduma ya kwanza.

Tukio hilo lilisaba-bisha Esma aache mambo yote na kuungana na wahudumu wa hoteli hiyo kumrudisha mama huyo kwenye hali ya uzima.

Akizungumza na paparazi wetu, Esma alisema mwanamke huyo hata yeye hamfahamu isipokuwa alikwenda na mama mmoja ambaye ndiye aliyemualika. “Duuuh! Jamani halafu nasikia ni mke wa mtu, sijui itakuwaje kwa mumewe maana bado hajazinduka,” alisema Esma wakati akizungumza na paparazi wetu. Hayo ni mambo matano tu kati ya mengi yaliyojiri kwenye pati hiyo.