NA EVELINA ODEMBA-OFISI YA DED SIKONGE.

WATU wawili raia wa Afrika Kusini wamefariki katika ajali ya ndege iliyotokea mapema asubuhi ya leo majira ya saa moja na nusu katika kata ya Igigwa Wilayani Sikonge.

Watu hao waliotambulika kwa majina ya D. Werner mwenye umri wa miaka hamsini na nane 58 pamoja na Werner Fredrick Fronaman mwenye umri wa miaka 36 wote wanamme na raia wa Durbun Afrika ya kusini walikuwa kwenye ndege yenye namba za usajili 19-ZU-TAF mali ya Afrika Kusini.

Akilezea tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Peres Magiri alisema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa tukio hilo na kusema kuwa watu hao walikuwa katika ziara ya kuhamasisha wanafunzi barani Afrika kusomea maswala ya Anga.

Kabla ya ajali kutokea Ijumaa walitua kwa dharula katika uwanja wa ndege wa Tabora wakitokea Entebe Uganda kuelekea Lilongwe Malawi ili kufika Afrika kusini. 

Jana asubuhi walipoanza safari, baada ya muda mchache walifanya mawasiliano na wataalamu wa uwanja wa ndege wa Tabora na kutoa taarifa kuwa injini ya ndege imezimika ghafla wakiwa angani hivyo wanafanya utaratibu wa kurudi Tabora.

Baada ya taarifa hizo hawakuweza kupatikana mpaka walipopata taarifa ya ajali hiyo na kufika wakakuta raia hao wameshafariki.