Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa onyo kali kwa Mkandarasi Urban & Rural Engineering, ambaye anatekeleza mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mkoani Kilimanjaro, kwa kumwambia asiijaribu serikali kwa kutikisa kibiriti kwani njiti zimejaa na kitawaka.Alitoa onyo hilo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya kazi kwenye Wilaya za Hai na Siha, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wao kuwa kasi ya mkandarasi huyo hairidhishi.Akizungumza katika mkutano na wananchi wa Hai, Naibu Waziri Mgalu alikiri mbele yao kuwa utendaji kazi wa mkandarasi husika unasuasua na zaidi ameonesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa serikali kwa kutoitikia wito alipoitwa kushiriki kwenye ziara hiyo pasipo kutoa sababu yoyote.

Akielezea zaidi, Naibu Waziri alisema yeye binafsi alijaribu kuwasiliana na mkandarasi huyo kwa njia ya simu pasipo mafanikio na hata ujumbe mfupi wa maandishi aliomtumia kumtaka apokee simu, haukujibiwa; kitendo ambacho alikiita ni dharau.

“Sasa mimi nataka nitoe salamu kwake. Mkandarasi Urban & Rural Engineering naona unatikisa kibiriti, unataka ujue kama kina njiti au hakina, na kama njiti zimejaa au zina baruti. Nataka nikwambie kibiriti kimejaa, njiti zina baruti na kitawaka.”

“Ulichokifanya ni dharau na unatupelekea tufanye maamuzi ya kuanza mapitio; na ni kweli nathibitisha ameshindwa kazi,” alisema Naibu Waziri.

Kufuatia hali hiyo, alimwagiza Msimamizi wa Mradi husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumjulisha mkandarasi huyo kwenda Dodoma mara moja kushiriki katika kikao kitakachofanya mapitio ya suala hilo ili ikibidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

“Kama ameshindwa kazi, tutawapatia wakandarasi wengine au hata TANESCO wanaweza kumalizia kazi husika.”

Awali, Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, alimweleza Naibu Waziri kuwa, Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Kilimanjaro unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania takribani bilioni 12.

Alisema, Mradi unahusisha ujenzi wa kilomita 150 za msongo wa umeme wa kilovoti 33, ujenzi wa kilomita 334 za msongo wa umeme wa kilovoti 400 na ufungaji wa mashine umba (transfoma) 132 na kwamba unatarajiwa kuunganishia umeme jumla ya wateja 3,572 katika vijiji 75 ndani ya mkoa.

Aliongeza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa mradi husika mkoani humo umefikia asilimia 43 hadi sasa.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika shule za msingi za Roo na Msamadi zilizopo wilayani Hai, pamoja na eneo la viwanda Mwangaza na shule ya msingi Gararagua wilayani Siha. Pia, alizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi wilayani Siha.