RASMI Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera amethibitisha kuwa ameliondoa jina la kipa wake, Klaus Kindoki katika usajili wao na kumpeleka kwa mkopo Lupopo FC ya DR Kongo.Kindoki anaondolewa Yanga kwa ajili ya kumpisha mshambuliaji mpya wa timu hiyo Mkongomani, David Molinga Ndama ‘Falcao’ akitokea Klabu ya FC Lupopo ya DR Congo kwa mkopo wa mwaka mmoja.Kipa huyo anatemwa Yanga kutokana na sheria za usajili za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambazo zinaruhusu wachezaji kumi pekee ambayo ilizidi kabla ya kumchomoa Kindoki.Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera alisema kuwa maamuzi ya kumuondoa Kindoki siyo ya ghafla na kushtukiza, awali yalikuwepo mazungumzo kati ya Lupopo na kipa huyo kabla ya kumtoa kwa mkopo.
Zahera alisema kuwa, Kindoki ameondoka baada ya kufikia muafaka mzuri kati na viongozi wa Yanga na Lupopo ya kukubali kumuachia mshambuliaji huyo kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake.“Niwaondoe hofu Wanayanga kuwa kabla ya kuja Falcao, nilikuwa nimeshazungumza na Kindoki juu ya yeye kumtoa kwa mkopo kwenda Lupopo aliyokuwa anaichezea awali. “Na uzuri yeye mwenyewe Kindoki alikubali kwa moyo mmoja kuondoka kwa mkopo kwenda Lupopo na Falcao kuchukua nafasi yake.“Hivyo, Kindoki rasmi anakwenda Lupopo kwa mkopo na Falcao anachukua nafasi yake baada ya makubaliano mazuri tuliyoyafikia pande zote mbili Yanga na Lupopo,” alisema Zahera. Kindoki amebakiza mkataba wa mwaka mmoja Yanga.