Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imesema hadi sasa jumla ya majeruhi 29 kati ya 47 waliopokelewa kutoka mkoani Morogoro Agosti 11 wamefariki dunia.


Kwa mujibu wa Msemaji wa Hospitali hiyo, Aminael Aligaisha mgonjwa Neema Shabani Chakachaka aliyekuwa na umri wa miaka 30 amefariki dunia alfajiri ya leo na Rosijo Mollel (35) alifariki dunia jana mchana saa nane.

Aligaisha ameongeza kuwa, majeruhi hao wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro waliolazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa sasa wamebaki 18 wote wakiwa bado wako katika Vyumba vya Uangalizi wa karibu (ICU).

Uongozi huo wa Muhimbili umesema mpaka sasa wagonjwa waliolazwa katika ICU wodi ya Mwaisela wamebaki 14, wengine watatu bado wako katika chumba cha uangalizi maalum cha Mwaisela (HDU Mwaisela) sanjari na mtoto aliyelazwa katika wodi ya uangalizi wa karibu ya watoto.