UWEZO wa Kiungo mshambuliaji wa Simba, Msudan, Sharaf Eldin Shiboub umempa heshima kubwa kwa wadau wa soka la Tanzania.Maujuzi aliyoonyesha kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumamosi huku akifunga mabao mawili ndiyo yamemfanya aonekana lulu.Simba chini ya mwekezaji wa mkuu wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ imempa nyumba ya kuishi maeneo ambayo ni tulivu na wanaishi watu wenye vipato vya juu.Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumamosi limezipata zimedai kuwa, Shiboub pamoja na nyota wengine wa kigeni kama vile Mkongomani, Deo Kanda na Mkenya, Francis Kahata wote wamepewa nyuma za kuishi maeneo ya Mbezi Beach.Asilimia kubwa ya maeneo hayo yanasifika kwa wakazi wao kuwa na kipato cha juu na huku pia wakazi wengi wa eneo hilo wakiwa ni raia wa kigeni (wazungu) hii ni kutokana kuwa na hali ya hewa nzuri, utulivu lakini pia yapo karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi.“Kwa hiyo wachezaji hao kwa sasa watakuwa wakiishi huko lakini pia uongozi unawatafutia nyumba wale Wabrazil katika maeneo hayohayo pia.“Kwa hiyo muda wowote kuanzia sasa nao watakuwa kwenye nyumba yao katika maeneo hayohayo. Sababu kubwa ya kuwapeleka huko ni kutokana na kuwa na utulivu hivyo uongozi unaamini kuwa itakuwa ni sehemu nzuri ya wachezaji hao kuishi kwa amani bila bugudha,”alisema.Championi lilimtafuta Mratibu wa Simba, Abbas Ally ili aweze kuthibitisha kuhusiana na suala hilo, alipopatikana alisema: “Ni kweli wachezaji hao wamepatiwa nyumba katika maeneo hayo, ambayo ni tulivu na yakayowewezesha kuishi kwa amani bila ya usumbufu.”