MWIMBAJI na prodyuza wa Nigeria, Solomon Oyeniyi, maarufu kama K-Solo, ametoa maoni yake kuhusu tishio la serikali nchini humo kumchukulia hatua mwimbaji  Augustine Kelechi, ajulikanaye kama Tekno.Wiki chache zilizopita Tekno amezua tafrani katika kitongoji cha  Lekki jijini  alipoonekana na wanawake waliokuwa wamevaa kihasara katika gari moja lililokuwa likipita mitaani humo ambapo baadaye ilikuja kujulikana kwamba tukio hilo lilikuwa linahusisha upigaji picha za video za wimbo wake wa  Agege.Katika video hiyo wanaonekana wanawake wakiwa nusu uchi wakicheza katika gari inayopita katika Daraja la Lekki-Ikoyi Link.Hali hiyo ilimfanya Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Sanaa na Utamaduni,  Olusegun Runsewe, aagize kufanywa uchunguzi wa tukio hilo akisema tabia ya Tekno ilikuwa inahatarisha usalama wa taifa hilo.Hata hivyo, akiongea na shirika la habari la  SUNDAY SCOOP, K-Solo, alisema serikali iangalie mambo yenye umuhimu wa kitaifa badala ya kumsulubu Tekno.