Maliha Mohammed mpishi maarufu kutoka Mombasa nchini Kenya amevunja rekodi ya dunia ya kitabu cha Guiness kwa kupika kwa muda mrefu zaidi.

Mwanamke huyo amekuwa mtu wa kwanza kuvunja rekodi hiyo barani Afrika.

Maliha alipika kwa muda wa saa 75 bila kusita na hivyobasi kuvunja rekodi ya dunia siku ya Jumapili katika hoteli ya kitalii ya Bay Beach mjini Mombasa.

Muda mrefu zaidi kuwahi kufikiwa ulikuwa muda wa saa 68 dakika 30 na sekunde 1, na ulivunjwa na Rickey Lumpkin mjini Los Angeles Marekani mwaka 2018.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 36 alikuwa ameandaa mapishi 400 ya nchini na kimataifa kwa ajili ya mashindano hayo ili kuweka jina lake katika kitabu hicho cha rekodi za dunia cha Guiness.

Vyakula alivyoandaa vitatolewa kwa nyumba za hisani na zile za mayatima kama mojawapo ya kutoa hamasa na kuwasaidia wasiojiweza mjini Mombasa.

Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho kupitia akaunti yake ya facebok ameandika ujumbe wa kumpongeza mwanadada huyo kwa hatua kubwa aliyofikia na si kwaajili ya Kenya pekee bali ni pamoja na bara zima la Afrika.