Na. Josephine Majura, WFM, Dodoma
SERIKALI imezindua rasmi Mpango Kazi wa Uendelezaji Miji Tanzania ili kuhakikisha nchi inakuwa na miji iliyopangwa na makazi yenye huduma zote za kijamii ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/17-2020/21.
Mpango huo umezinduliwa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango kazi huo, Waziri Jafo alisema kuwa Serikali imejidhatiti kuandaa mipango miji madhubuti ambayo imezingatiwa katika miongozo ya kuandaa mipango ya taifa.
“Serikali inazindua rasmi Mpango huo ili kuleta mpangilio mzuri wa Miji wenye manufaa kwa Taifa na kufanya ukuaji wa miji kuwa mchakato wenye manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa nchi”, alisema Waziri Jafo.
Waziri Jafo alisema kuwa mpango huo umejikita katika maeneo manne ambayo ni matumizi ya lugha ya mpango kazi, suala la utawala na kanuni, mkakati wa fedha pamoja na kuchunguza njia za kukuza uchumi kwa kutambua njia ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi katika viwango vya juu.
Alisema kuwa maeneo hayo manne ni muhimu kufanya ukuaji wa miji kuwa mchakato wenye manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa kuwa unatoa mapendekezo ya msingi kwa wakati ambayo ni muhimu kwa upangaji wa maendeleo ya miji nchini.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula, alisema kuwa ukuaji wa miji ni suala pana ambalo linahitaji wadau wengi kuunganisha juhudi ili kuhakikisha ukuaji wa miji inayosimamiwa kikamilifu.
Dkt. Mabula amesema kuwa, wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano katika kuleta pamoja jitihada za kila taasisi ili kuepuka jambo moja kufanywa na wadau zaidi ya mmoja, lengo likiwa kufanikisha malengo ya nchi iliyojiwekea.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolph Ndunguru, aliwashukuru viongozi na wote waliohudhuria katika hafla hiyo muhimu kwa Taifa na kueleza kuwa mpango huo utasaidia kutatua changamoto za upangaji miji kwa maendeleo ya uchumi na Taifa kwa ujumla.
Vilevile Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa kiuchumi na Kijamii, Dkt. Tausi Kida, amesema Mpango huo utasaidia katika uandaaji wa mipango ya kitaifa ya uendelezaji miji pamoja na uandaaji wa sera kwa kuwa uliotokana na utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii kwa kuwa uliofanywa kwa kufuata kanuni za kisayansi za ufanyaji tafiti.