NA MWAMVUA MWINYI, PWANI.

MWAJUMA Omary Malembeka (28) anadaiwa kumuua mume wake Selemani Kondo (43) mkulima na mkazi wa Chamalale, kata ya Vihingo, Mzenga, wilayani Kisarawe mkoani Pwani, kwa kumchoma na bisibisi kwenye bega.

Akithibitisha kuhusu tukio hilo,kamanda wa polisi mkoani hapo, Wankyo Nyigesa alisema mwanamke huyo alifanya maamuzi hayo kutokana na wivu wa kimapenzi.

Alieleza, kulikuwa na mzozo baina yao ambapo Mwajuma alimtuhumu mume wake kuwa siyo mwaminifu katika ndoa yao.

“Selemani aliuawa kwa kuchomwa bisibisi katika bega lake la kushoto na sehemu ya juu na mke wake huyo”alifafanua.

Wankyo alisema, kujichukulia sheria mkononi sio jambo la msingi kwani inaweza kuleta madhara kama ya kujeruhi ama kusababisha kifo ,na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.