Tanzania na Misri zimeanza mikakati ya uwekezaji katika sekta ya ngozi nchini, ambapo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amekutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Misri ambao wamefika nchini kwa nia ya kuwekeza katika sekta ya ngozi.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dodoma, Ulega amesema kuwa tayari wameshakubaliana baadhi ya mikakati ili uwekezaji watakaoufanya nchini uwe na tija kwa pande zote mbili.

Amesema kuwa ujio wa wawekezaji hao wakubwa kutoka nchini Misri, ambao umeongozwa na mshauri wa waziri wa viwanda na biashara wa nchi hiyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Kiwanda cha kuchakata Ngozi, Cairo for Investment and Development, Yasser El Maghraby, umeonyesha utayari mkubwa wa kuwekeza hapa nchini katika sekta ya ngozi kutokana na uwepo wa ngozi nyingi na bora.

“Tumepata wageni ambao wamekuja kuona maendeleo ya sekta ya ngozi nchini wawekezaji hawa ni wakubwa katika biashara ya ngozi nchini Misri, sisi kama taifa bado hatujafaidika vya kutosha na zao la ngozi, tumekuwa tukizalisha takribani vipande vya ngozi ya ng’ombe milioni nne na mbuzi milioni tano kwa mwaka, lakini kuvibadilisha kuviweka katika bidhaa mbalimbali kama vile viatu, mabegi na mikanda bado ni changamoto,”amesema Ulega

Aidha, Ulega amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa jitihada anazozifanya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda vinavyochakata mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi.

Amefafanua kuwa ziara ya wawekezaji hao wakubwa katika biashara ya ngozi nchini Misri, Mahmoud Sargy Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi, Sargy Tannery na Hisham Gazar Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi, Piel Color ni mwendelezo wa nchi ya Misri na Tanzania kuwa katika historia na mahusiano mazuri.

Pia, Ulega ameishukuru serikali ya Misri kwa kutuma timu hiyo ya wawekezaji ikiongozwa na mshauri wa waziri wa viwanda na biashara nchini humo kufuatia ziara ya kikazi iliyofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa nchini Misri kuanzia tarehe 8 hadi 10 Mwezi Julai Mwaka 2019 ambapo alitembelea mji wa viwanda vya ngozi Roubiki na kuzungumza na wazalishaji wa bidhaa za ngozi nchini huu

Mmoja wa wawekezaji hao kutoka Misri, Mahmoud Sargy ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuchakata ngozi, Sargy Tannery ambacho ni moja ya viwanda vinavyosafirisha kwa wingi ngozi kwenda nje ya nchi ameiomba serikali ya Tanzania kuendelea kuunga mkono sekta binafsi na kwamba ili waweze kunufaika kupitia uwekezaji ambao wataufanya hapa nchini, wanatarajia serikali itawawekea mazingira mazuri ya uwekezaji ili uwe na tija kwao na taifa