Hamisi Singa (30), raia wa Burundi na Watanzania wanne wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba, likiwemo la kuingilia mfumo wa taarifa za miamala ya fedha za mawakala  na kutakatisha fedha Sh26 milioni.

Mbali na Singa  ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo,  washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 72/2019  ni Jailos Joseph, Singa Mnunga, Japhet Mkumbo na Omari Omari.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salim Ally.

Wakisomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, ilidaiwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka saba likiwemo moja la kutakatisha fedha.

Alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa tarehe isiyofahamika kati ya Januari na Julai, 2019 maeneo ya Arusha, Manyara na sehemu nyingine nchini walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka la pili washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho kwa ulaghai walijipatia Sh 26,432,441 kwa kuhamisha fedha hizo kutoka kwa wateja wa Vodacom na Airtel.

Washtakiwa wanadaiwa katika shtaka la tatu walisambaza ujumbe usemao ‘Tuma pesa kwenye namba hii’ huku wakijua ujumbe huo wa uongo wenye nia ya kupotosha umma.

Shtaka la nne kwa washtakiwa wote, wadaiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwa watu mbalimbali ukielekeza kutuma fedha kwenye simu iliyosajiliwa kwa majina mengine.

“Mheshimiwa Hakimu shtaka la tano lina wakabili washtakiwa wote wanadaiwa kusambaza ujumbe wa uongo kwa nia ya kujipatia fedha.

“Shtaka la sita linamkabili mshtakiwa Hamis, anadaiwa akiwa mwajiriwa wa Kampuni ya Tigo kwa ulaghai alipata uwezo wa kuingilia miamala ya fedha ya mawakala wa tigo kwa nia ya kujipatia fedha.

“Shtaka la saba kwa washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh 26,432,441 huku wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu,”alidai Wankyo.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu kesi hiyo imefunguliwa chini ya sheria ya Uhujumu Uchumi ambapo mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Kesi itatajwa Agosti 15 mwaka huu.