Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta amesema, kilichocheleweshwa kuanza kwa ujenzi wa ufukwe mpya wa Coco ni kufuatwa kwa sheria za manunuzi pamoja na mabadiliko ya mchoro uliosababishwa na ujenzi wa daraja la Selander.


Sitta ameyabainisha hayo kufuatia agizo lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuitaka na kuipa Manispaa hiyo mwezi mmoja ili ihakikishe inaanza ujenzi wa  mradi huo mara moja.

''Hii miradi ya mkakati tunafuata sheria 'to the dot' maana yake ukikosea kidogo mkandarasi mwingine anaenda kukata rufaa na wakikata rufaa mnaweza kukaa siku tisini zingine sababu sheria hazikufuatwa, lakini vilevile inaweza kuonekana mnafuata matakwa yenu binafsi, kwahiyo sheria zetu za manunuzi zinatubana sana kwahiyo muda wote ambao mmeona umechelewa ni taratibu na sheria za manunuzi'', amesema Meya Sitta.

Mradi wa ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 14 na tenda ya kumtangaza mkandarasi atakayeanza ujenzi huo  itatangazwa Agosti 19, 2019, ili kuanza ujenzi huo mwishoni wa mwezi huu na ujenzi utakaochukua miezi sita.