Mchungaji wa Mitume na Manabii, Daudi Mashimo, baada ya kumaliza maombi aliyokuwa akimuombea mwigizaji wa filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu ambaye kwa sasa mambo yanamuendea vizuri, amesema ameandaa maombi maalum ambayo yataanza wiki ijayo kwa ajili ya kumuombea mwigizaji wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ili aingie kwenye ndoa haraka.  Mashimo aliliambia Gazeti la Ijumaa kuwa aliwahi kuongea na Lulu kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo alimuuliza kama ameshafunga ndoa, lengo lilikuwa ni kupata ufahamu zaidi wa hilo ili amfanyie maombi maalum.

“Mwanzo nilidhani ameshaolewa kwa sababu watu walidai kuwa aliolewa, lakini nilipobaini bado hajaolewa ndiyo nikaamua kumuuliza mwenyewe ambapo alidhihirisha kwa maneno ya Biblia kuwa hajaolewa, sasa nimeandaa maombi maalum ambapo nitaweka wazi kama ilivyokuwa kwa Wema,” alisema Mashimo.

Mchungaji huyo aliongeza kuwa, aliamua kuchukua jukumu hilo kwa sababu Lulu ni mdogo wake wa muda mrefu na wamekuwa pamoja kwenye tasnia ya filamu tangu wakiwa kwenye Kundi la Kaole Sanaa. “Mimi na Lulu tumekuwa pamoja kwenye tasnia tangu enzi za Kaole hivyo nimeamua kusimama na yeye na kwa uwezo wa Mungu ataolewa haraka,” alisema Mashimo.

Mashimo alimalizia kuwa ataanika maombi hayo ambayo yataanza rasmi wiki ijayo na ni maombi mema kwani uchumba hautakiwi kuwa wa muda mrefu. “Muda aliokaa Lulu kwenye uchumba sasa unatosha hivyo maombi nitakayompigia na mfungo hakika ataolewa haraka sana Mungu ni mwema,” alisema Mashimo.