Mbunge wa Baraza la Wawakilishi nchini Marekani, Rashida Tlaib amepewa sharti zito kutembelea Palestina baada ya waziri wa mambo ya nje wa Israel kutangaza zuio la wabunge wawili wa chama cha Democratic kufanya ziara nchini Israel pamoja na Palestina.

Sharti hilo limetangazwa masaa machache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Israel kusema kuwa itamruhusu mbunge mmoja kuzuru Palestina kumuona bibi yake kwa sababu za kibinadamu.

Katika ujumbe wa kijamii Ijumaa asubuhi, Tlaib aliandika hatua hiyo ingemuumiza sana kama angezuiwa hata kumuona bibi yake.

“Uamuzi huu unatokana na kuzingatia kuwa kumtembelea bibi yangu chini ya hali hizi kandamizi ni kinyume cha kile ambacho nina imani nacho, vita dhidi ubaguzi, ukandamizaji na dhulma,” aliandika Tlaib katika barua aliyoituma kwa waziri wa mambo ya ndani wa Israeli, Aryeh Deri akiomba kuruhusiwa kumuona bibi yake

Aidha, Katika barua yake, Tlaib amesema kuwa ataheshimu na kutii makatazo yote aliyopewa na hatahamasisha migomo dhidi ya Israel.

Mapema Ijumaa Israel ilibadilisha msimamo wake kuhusu wabunge wanawake wawili wa Marekani ambao ni Ilhan Omar na Rashida Tlaib iliwazuia kuingia nchini humo na baadaye kumruhusu mmoja wa wabunge hao, Tlaib kuingia nchini humo.

Barua iliyoandikwa na ofisi ya wizara ya mambo ya ndani ya Israel, imesema kuwa mbunge huyo atalazimika kuheshimu vizuizi vyote atakavyowekewa na hataruhusiwa kueneza misimamo pingamizi wakati wa ziara yake dhidi ya Israel.