Na Mwandishi Wetu.

WANANCHI wa Jimbo la Manonga lililopo katika Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wamempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Seif Gulamali kwa hatua anazozichukua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali jimboni humo zikiwemo za kielimu na upatikanaji wa huduma za afya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo iliyofanywa na Mbunge huyo jimboni humo ,wananchi hao mbali na pongezi kwa Mbunge huyo, pia walieleza kuridhishwa na kasi ya ukuaji wa maendeleo inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano na kumuomba mbunge huyo kuwafikishia salamu zao kwa Rais John Magufuli.

Wakizungumzia mafanikio hayo, wananchi hao walisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Jimbo la Manonga limepiga hatua kubwa za kimaendeleo na hivyo kuleta ustawi wa maisha kwa wananchi wote kutokana na uwepo wa huduma za uhakika za afya, maji, miundombinu ya barabara pamoja na ujenzi wa shule na vyumba vya madarasa katika vijiji mbalimbali.

 Mmoja wa wananchi hao Masoud Elias kutoka Kata ya Mwamala alisema Mbunge amekuwa chachu ya maendeleo ya Jimbo hilo na hasa baada ya kutekeleza ahadi mbalimbali alizozitoa wakati wa kampeni zake za Mwaka 2015 jambo alilosema kuwa hujitokeza mara nyingi hasa pale viongozi wanapokuwa wameshaingia madarakani.

Akizungumzia ujenzi wa vituo vya afya katika Jimbo hilo, Masoud alisema mbunge huyo kwa hamasa yake amewezesha kupatikana kiasi cha Sh Milioni 10 kwa kila zahanati iliyopo katika Jimbo hilo zilizotolewa na Mfuko wa RBF huku wakijiandaa kufungua zahanati mpya katika vijiji vya Itale, Bugingija, Chapela pamoja na kijiji cha Imalilo kilichopo jimboni humo.

Alisema pamoja na ujenzi wa zahanati hizo, Mbunge huyo pia ameweza kununua gari maalumu kwa ajili ya kubebea wagonjwa katika kituo cha afya cha Simbo na kuwezesha huduma ya upasuaji katika kituo cha afya cha Choma na hivyo kuwa msaada baada ya Hospitali ya Igunga ambayo ilikuwa na jukumu hilo pekee katika suala zima la huduma ya upasuaji.

“Ukweli ni kwamba hivi sasa changamoto ya ukosekanaji wa huduma za afya katika vijiji mbalimbali ndani ya Jimbo letu imekuwa siyo tatizo kubwa kwa kuwa maeneo mengi yana vituo vya afya lakini hata huduma zinazotolewa kwa kiasi kikubwa zimekuwa bora, pongezi hizi pia zimfikie Rais John Magufuli kwani kasi yake ya kutuletea maendeleo inaungwa mkono kwa vitendo na Mbunge huyu” alisema Masoud.
Kwa upande wake mkazi wa Kata ya Ziba Shaaban Magengeni alisema kupitia mpango ulioanzishwa na Mbunge huyo wa kuwasomesha wanafunzi wa Jimbo hilo kwa elimu ya kidato cha tano hadi cha sita, umeweza kuleta matokeo mazuri ya ufaulu kwa watoto wao na kuipaisha Manonga kielimu tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Alisema mpango wa utoaji wa elimu bure chini ya agizo la Rais John Magufuli kwa kiasi kikubwa umesaidia kupatikana wahitimu wengi ambao hujikuta wakibaki mitaani kwa kukosa ada za kuendelea kidato cha tano na sita suala walilodai kuwa Gulamali aliliona na kuamua kulifanyia kazi kwa kuwasomesha wanafunzi wote wanaofaulu.

“Tunamshukuru kwa hatua hii, hivi sasa tunajivunia matokeo mazuri ya ufaulu wa kidato cha nne kwa wanafunzi katika shule yetu ya Ziba na kuifanya kuongoza kiwilaya katika mitihani mbalimbali ukiwemo wa taifa, tuzidi kumuomba Mbunge aweze kuendelea na mpango huu kwa kuwa unaleta akisi ya kimaendeleo” Magengeni.