Mawakili wanne wanatarajiwa kuanza kumtetea aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu  aliyevuliwa wadhifa huo hivi karibuni.

Lissu yuko nchini Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, alifungua rasmi shauri hilo jana.

 Alute Mughwai kaka yake Lissu akizungumza na waandishi wa habari  amesema kesi hiyo itaanza kuunguruma Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Mawakili hao wataongozwa na Kibatala na wengine ni Jeremia Mbesya, John Malya na Fredi Kalonga.

Amebainisha kuwa maombi ya kufunguliwa kesi hiyo  chini ya hati ya dharura, kupitia kwake (Mughwai) aliyempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, yatasikilizwa Agosti 21, 2019.

Mughwai  amesema wanatarajia Lissu kurejea Tanzania Septemba 7, 2019 baada ya uchunguzi wa mwisho wa madaktari wake utakaofanyika Agosti 20, 2019.