OFISAHabari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire ametamba kuifunga Yanga pindi watakapokutana katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar, kesho Jumatano.

Ruvu Shooting itapambana na Yanga ambayo Jumamosi iliyopita ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Township Rollers katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na hivyo kusonga raundi ya kwanza katika michuano hiyo.

Bwire ameliambia Championi Jumatatu kuwa: “Tumejiandaa vyema kuwakabili Yanga wanaojiita wa kimataifa, tunahitaji ushindi licha ya kwamba wameshinda huko Botswana, sisi tutawaharibia furaha yao ya ushindi.

“Unajua Botswana labda hawaifahamu Yanga kama tunavyoifahamu sisi, kama hawatojali watoke Botswana waje Uhuru kuangalia jinsi gani tutakavyoshinda,” alisema na kuongeza:

“Wachezaji wetu wana morali kubwa kwa ajili ya kupata ushindi, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani kuona namna tutakavyotoa burudani.” Msimu uliopita, Yanga iliifunga Ruvu Shooting mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara.