KIPA namba moja wa simba, Aishi Manula amekiri kuwa kiwango cha kipa mwenzake, Benno Kakolanya kipo juu na anaamini atakuwa na msaada mkubwa katika kuiwezesha timu hiyo inayofundishwa na Mbelgiji, Patrick Aussems kupata mafanikio.Kauli hiyo aliitoa juzi mara baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii kumalizika uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Azam FC kwa Simba kushinda mabao 4-2.Katika mchezo huo, Kakolanya alikaa langoni kutokana na Manula kupata majeraha akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars ilipokuwa inajiandaa na mchezo wa kufuzu Chan na Kenya.


Akizungumza na Championi Jumatatu, Manula alisema ana kubali kiwango cha Kakolanya huku akifurahi uwepo wake katika kikosi hicho. Manula alisema kuwa ana fahamu uwezo wa kipa huyo tangu akiwa Yanga, hivyo hana hofu naye zaidi akipanga kumpa ushirikiano mkubwa katika timu hiyo.“Hata Ally Salim naye yupo vizuri ndiyo maana amesajiliwa nikiwepo mimi langoni, nisipokuwepo hakuna kinachoharibika, kwa sasa bado naendelea na matibabu hivyo sina uhakika kama nitadaka mchezo wa marudiano dhidi ya UD Songo.“Lipo wazi kabisa kuwa Kakolanya ni kati ya makipa bora hapa nchini ambaye aliwahi kucheza timu ya taifa, hivyo sina hofu na kiwango chake kabisa.“Ninafuraha kucheza naye katika timu moja na kikubwa namuahidi kumpa ushirikiano tukiwa hapa Simba,” alisema Manula ambaye anasumbuliwa na majeraha ya nyonga akiwa amekosa michezo miwili ya kiushindani, ule wa kimataifa dhidi ya UD Songo na huo wa juzi.Simba itarudiana na UD Songo wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa ikiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.