Idadi ya wacheza kamari wanaolalamika kuhusu makampuni ya kamari ya Uingereza imepanda kwa karibu asilimia 5,000 katika kipindi cha miaka mitanoiliyopita

Kulikuwa na malalamiko 8,266 mwaka jana, rekodi iliyokusanywa na tume inayohusika na michezo ya kamari, ikilinganishwa na malalamiko 169 mwaka 2013.

Malalamiko mengi yalihusu makampuni kukataa kulipa washindi au kushindwa kufanya kazi katika hali ya kuwajibika ipasavyo.

Ongezeko hilo limekuwepo kutokana na ongezeko kubwa la michezo hiyo ya kamari nchini Uingereza.

'Ishara nzuri'
Makampuni makubwa ya kamari yameahidi kutenga pauni milioni 60 kwa mwaka kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wacheza kamari na kusema kuwa wanafanyia kazi mpango wa kupunguza athari zitokanazo na kamari.

Neil McArthur, mkurugenzi wa tume ya udhibiti wa michezo ya kamari, amesema kuna sababu za ongezeko la malalamiko hayo.

''Tunalazimisha soko la michezo ya kamari kufahamu wateja wake, na hii pengine ni ishara njema kwa sababu inawafanya wateja kutaka uwepo usimamizi zaidi na ningependa waendelee kufanya hivyo,'' alisema.

Soko limetanuka kwa haraka sana tangu serikali ilipopunguza vikwazo kwenye soko la kamari na matangazo mwaka 2007.

Wacheza kamari kwa sasa wanapoteza karibu mara mbili zaidi ya makampuni ya kamari yalivyokuwa yakipoteza miaka 10 iliyopita. Mwaka jana, wacheza kamari walirekodiwa kupoteza kiasi cha pauni bilioni 14.5.

Ongezeko kubwa liko kwenye kamari inayochezwa mtandaoni, ambapo michezo mipya imewavutia wateja wapya.

Wakurungenzi wa makampuni ya kubeti wafurushwa


Je michezo ya kamare inaleta hofu gani katika mataifa ya Afrika mashariki?
Amanda, (si jina halisi) , alikuwa kwenye miaka ya 50 alipoanza kucheza kamari mtandaoni katika mtandao wa Jackpotjoy.

Alicheza kamari na pesa zake zote. Baba yake alipofariki, alirithi nyumba, na nyumba yenyewe pia aliipoteza kwenye kamari.

Kwa ujumla, Amanda alipoteza pauni 633,000. Mara ya mwisho alicheza kamari siku ya mwisho ambayo ndio alifanywa kuwa mufilisi.

''Nilikuwa nakaa mtandaoni na kubofya kwenye kompyuta'' Alisema ''Hata nilipoacha kucheza kwa siku moja, haraka sana nilitumiwa barua pepe kushawishiwa kuendelea kucheza''.

Haki miliki ya pichaJACKPOTJOY
''Ni jambo baya sana nililojifanyia kwa kweli. Kilakitu nilichokifanyia kazi. Watoto wangu wananitegemea na sasa nimeuharibu urithi wao.''

Jackpotjoy wamesema imekuwa ikifanya kazi kwa kufuata taratibu za mamlaka

Mashine za kamari ambazo zimekuwa na hatari kwa watu kupoteza fedha zao, zimepigwa marufuku, lakini hakuna zuio kama hilo kwenye mitandao ya michezo ya kamari. Hii ina maanisha kuwa wateja hupoteza maelfu ya pauni kwa dakika chache.

Wanaharakati wanasema serikali inahitajika kuwajibika zaidi ili kuwalinda watu wanaocheza kamari.

'Tatizo'
Daniel Clinkscales alikatisha uhai wake akiwa na miaka 35 baada ya kupambana na uraibu wa kamari kwa miaka kadhaa.

Alikuwa meneja mauzo ambaye alikuwa akilipwa vizuri sana, lakini alitafuta kazi nyingine mbili ili aweze kugharamia tabia yake ya kucheza kamari.

Mama yake, Jo Holloway, anasema Daniel alikuwa akicheza mchezo huo kwa kujificha kwa miaka mingi.

''Nafikiri alishindwa kukubaliana na ukweli kuwa alikuwa mwerevu, mwenye uwezo, na mwenye mafanikio makubwa katika karibu kila jambo anapoweka mkono wake- alikuwa na tatizo moja. Kucheza kamari.'' Alisema mama yake Daniel.

Anafikiri kuwa mzigo wa uwajibikaji upewe kwa makampuni ya kamari, Kwasababu wacheza kamari wengi hawajui jinsi ya kuacha.

''Kucheza kamari kumefanywa kuwa kwa kawaida sana, mithili kitu ambacho hufanywa bila kutambua. Lakini si hivyo. Unaweza kupoteza nyumba yako siku moja. Jambo hilo liwe na madhara kiasi gani kabla ya watu kuchukua hatua?''

Tume inayosimamia michezo ya kubahatisha imesema waratibu wana taarifa za kutosha kuhusu kuhakikisha usalama wa wanaocheza kamari, na kuhakikisha wanacheza na fedha ambazo hazitawagharimu kiuchumi iwapo watazipoteza.

Makampuni makubwa ya kubeti yameridhia kuongeza ujumbe wa kutahadharisha kuhusu michezo ya kamari katika matangazo yao ya biashara.