Na Suleiman Msuya.

KAMPUNI ya Kuzalizsha Chai Kagera (KTCL) imesema itatumia wiki ya viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kutangaza bidhaa yao mpya ya Yetu Chai.

Hayo yamesemwa na Meneja Msimamizi wa Mipango na Biashara wa Yetu Chai, Fredson Simon wakati akizungumza na Tanzania Daima. 

Simon alisema wamejipanga kutumia fursa ya wiki ya viwanda SADC kutangaza na kuelezea bidhaa hiyo mpya ya Yetu Chai ili nchi wanachama waweze kuifahamu.

Alisema kupitia mkutano huo watapanua soko la bidhaa yao na kuongeza wateja hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na wananchi.

"Sisi KTCL kupitia bidhaa yetu mpya na Yetu Chai na zingine tutahakikisha mkutano huu wa SADC unatopanulia soko la bidhaa zetu," alisema.

Meneja huyo alisema kwa sasa soko lao kubwa lipo nchini Kenya na Rwanda ambapo kwa sasa wanajipanga kuelekeza nguvu zao nchini Mauritius, Comoro, Afrika Kusini na Zambia.

Aidha, alitoa rai kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Kitanzania kutumia fursa hiyo ya mkutano wa SADC kutangaza bidhaa na kujitangaza katika ukanda huo.

Alisema iwapo Watanzania watajipanga vizuri kupitia maonesho hayo ya wiki ya viwanda watanufaika.

Simon alisema wamekuwa wakishindwa kushiriki mikutano mikubwa kama hiyo hivyo wakati ni sasa.

Wiki ya viwanda ya SADC itaanza Agosti 4 hadi 8 mwaka huu ambapo wafanyabishara na wamiliki wa viwanda kutoka nchi 16 wanatarajiwa kushiriki.