Klabu ya Arsenal imemuuza beki wake wa kati na nahodha wa timu hiyo, Laurent Koscielny kwenda klabu ya Bordeaux kwa dau la Euro milioni 5.

Mchezaji huyo mwenye miaka 33 anarejea katika ligi ya Ufaransa baada ya miaka tisa ya kucheza ligi kuu ya Uingereza katika klabu ya Arsenal.

Koscielny alikuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Arsenal yenye maskani yake jijini London, ambapo ilitaka mchezaji huyo aendelee kubaki klabuni hapo.

Mchezaji huyo aling’ang’ania kuuzwa na kugoma kusafiri na timu kwenda kwenye ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Marekani.

“Tumekubali uhamisho kwenda Bordeaux baada ya kuafikiana vyema kuhusu vigezo vya usajili, tunamshukuru Laurent kwa mchango wake mkubwa katika klabu hii na tunamtakia kila la kheri katika maisha yake ya baadaye,”imeeleza taarifa kutoka klabu ya Arsenal

Aidha, Koscielny alikataa mkataba mpya na Arsenal, maarufu kama ‘The Gunners’ baada ya kuona kuwa vipengele vya mkataba huo vinapunguza mchango wake na uwezo wake wa baadaye klabuni hapo.

Koscielny alijiunga na Arsenal mwaka 2010 na kuchezea miamba hiyo zaidi ya mechi 300.

Hata hivyo, kwasasa klabu ya Arsenal inapambana kumsajili beki mpya wa kati kabla ya dirisha la usajili la Ligi Kuu ya Uingereza kufungwa Alhamisi saa 11 jioni nchini humo