Kenya imeishinda Djibouti na kupata kura ya Umoja wa Afrika ambayo inatarajiwa kuongeza chachu ya kampeni ya nchi hiyo kuwa mjumbe asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imesema kuwa, Kenya imepata kura 37 dhidi ya 13 za Djibouti wakati wa uchaguzi ulioandaliwa na Kamati ya Kudumu ya Wawakilishi ya Umoja wa Afrika uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Aidha, Kenya inatarajiwa kuungana na Niger na Tunisia ambazo zilichaguliwa mwezi June kuwa wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameupongeza Umoja wa Afrika kwa kuidhinisha nia ya Kenya ya kuwa na nafasi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kuzitaka nchi nyingine wanachama wa Umoja huo kuiunga mkono Kenya kupata nafasi hiyo.