Msanii mkongwe wa maigizo nchini Tanzania, Johari, amefunguka suala la Wema Sepetu kutoonekana na kususia vikao au mikutano ambayo inayohusisha wasanii wa filamu.
Johari amejibu tuhuma hizo akisema kuwa Wema anafanya hayo kutokana na wasanii wa Bongo Movie kutoonesha msaada au ushirikiano wowote wakati yupo katika kipindi cha matatizo ya kisheria.
Akizungumza na EATV & EA Radio Digital Johari amesema, “sijajua kama hiyo ndiyo sababu ya Wema Sepetu kususia vikao, hivyo siwezi kuingilia ni vitu vya mtu binafsi lakini naweza kusema siku ambayo alipelekwa mikononi mwa sheria labda watu hawakuwa na taarifa".
"Mimi binafsi wakati anapata hayo matatizo nilikuwa nimesafiri na sikuweza kwenda eneo la tukio”, ameongeza Johari.
Aidha msanii huyo amesema kuwa yeye binafsi huwa anaongea naye vizuri, anampigia simu na haoni kama ana tatizo. Pia Johari ameongelea kuhusu ujio wa kazi yake mpya itakayotoka hivi karibuni ambayo itahusu maisha yake.