Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzana ( TRA), limekamata katoni 230 za aina 11 tofauti ya vipodozi vyenye viambata vya sumu ambavyo vimepigwa marufuku kuingia nchini.

Vipodozi hivyo vilikuwa vikisafirishwa kwa njia ya magendo kwa kuchanganywa na mchanga wa shaba kutoka Zambia kwenda jijini Dar es Salaam.

Kukamatwa kwa shehena hiyo katika eneo la Chamwino katika, Manispaa ya Morogoro, barabara kuu ya Iringa-Morogoro, kumetokana na taarifa zilizopatikana kutoka kwa raia wema kwa polisi waliokuwa doria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha kukamatwa kwa vipodozi hivyo Julai 30, mwaka huu, majira ya saa sita usiku, vikiwa kwenye maboksi yaliyoviringishwa karatasi za nailoni.

Mutafungwa alisema vipodozi hivyo vilikamatwa vikiwa kwenye lori lenye namba za usajili T 367 AXY aina ya Scania, mali ya kampuni ya usafirishaji ya Thornswift ya jijini Dar es Salaam.

"Walichofanya wasafirishaji ni kuchanganya maboksi haya yenye vipodozi vilivyopigwa marufuku na mchanga huo wa shaba uliokuwa kwenye kontena, ambao ulikuwa ukisafirishwa kutoka Zambia kwenda Dar es Salaam na baadaye China," alisema.

Akavitaja vipodozi vilivyokamatwa na kiasi cha katoni kwenye mabano kuwa ni Teint Clair (86), Bronze Tone Cream (31), Perfect White Cream (32), Perfect White Lotion (15) ,sabuni ya Perfect White (12), Carot Cream (18), Diana Lotion (12), Coco Pulp Cream (14), Actif Plus Cream (10) na Extra Clair katoni nane.

Aliwataja waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo kuwa ni dereva wa gari, Sudi Ally (60) mkazi wa Kongowe Mzinga jijini Dar es Salaam, ambaye awali inadaiwa alijaribu kutoroka na kulitelekeza lori hilo, lakini alitiwa mbaroni baada ya kufanyika msako, Samson Mhabe (22) dereva na mkazi wa Tunduma mkoani Songwe, ambaye alikuwa msindikizaji wa mzigo huo uliokamatwa.

"Watuhumiwa walidai vipodozi hivi walivipakia baada ya kuvuka mpaka wa Tunduma upande wa Tanzania na tunawashikilia pamoja na gari lililokamatwa likisafirisha bidhaa hizi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani kwa kushirikiana na TRA na TBS (Shirika la Viwango Tanzania)," alisema.