Nyota anayetamba na ngoma ya Tetema, Raymond Shaban Mwakyusa ametolea ufafanuzi kauli yake kuwa ni msanii wa Tip Top Connection na kusema kuwa hakumaanisha kuwa ameondoka kwenye lebo ya Wasafi isipokuwa alimaanisha kuwa yeye ni moja ya wanafamilia wa Tip Top kutokana na kuishi nao vizuri kwa kipindi chote alichokuwa nao.

Rayvanny amesema hayo huku kukiwa na tetesi kuwa msanii mwingine wa WCB Harmonize anataka kujiengua kutoka lebo hiyo huku ikielezwa kuwa ameanzisha lebo yake ya Konde Gang.

“Nimesema nipo Tip Top kwa sababu bado ni familia yangu, nipo Ya Moto Band pia kwa sababu Mkubwa na Wanawe bado familia yangu. Lakini sijasema nipo sipo Wasafi kwa sababu nipo Tip Top , no, no, no,” amesema Rayvanny.

Amesema Babu wa Tale Tip Top ndiyo Babu Tale wa Wasafi, Diamond wa Tip Top ndiyo Diamond wa Wasafi, Mkubwa na Wanawe pia.

Ameongeza kuwa wao ni familia moja. wametoka mbali, wana umoja na wanapendana sana ndiyo maana wanapata mafanikio makubwa kutokana na kazi zao kukubalika sana kwa watu.

“Mimi ninatoa tu angalizo. Kama tukiendelea kupendana, Wasafi itadumu sana na wataongezeka wengine na watafika mbali zaidi. Sisi sio wasanii wa mwisno, kuna wasanii wengi sana watafika Wasafi. Mimi natamani Wasafi ije kuwa kama Sony na Universal.”