Dar es Salaam. Kuna ukweli wowote kuhusu habari zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa msanii Harmonize amejiengua katika lebo ya Wasafi inayoongozwa na Diamond Platnumz.

Hakuna anayejua hilo lakini kuna baadhi ya kauli  zilizotolewa na Diamond mwenyewe na mmoja wa mameneja wake zinaweza kutoa picha ingawa hakuna kati yao aliyethibitisha kuwa Harmonize ameachana na lebo hiyo.

 “Kama Harmonize anataka kuondoka aondoke,” alinukuliwa akisema Diamond na baadaye kauli hiyo kuungwa mkono na mmoja wa  mameneja wa Wasafi, Said Fella, “Kama akiamua kuondoka hakuna wa kumzuia.”

Huo ni mwanzo wa kile kinachodaiwa Harmonize anaweza kujitoa kwenye lebo ya Wasafi.

Lakini mara kadhaa Harmonize amekuwa akijibu kuhusu tetesi hizo, “Siwezi kuondoka Wasafi kwani namchukulia  Diamond kama baba yangu ndio aliyenilea kimuziki.”

Tayari Harmonize anamiliki lebo ya muziki ya Konde Gang ambayo inafanya kazi zake kama ilivyo Wasafi.