ACHANA na gumzo lake la kudaiwa kujitoa kwenye lebo iliyomlea kimuziki ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, gumzo lingine jipya la staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ ni juu ya kuombwa kugombea na kuwa mwakilishi wa watu bungeni. Miezi kadhaa iliyopita, baadhi ya wanakijiji wa Mahuta, Tandahimba mkoani Mtwara, sehemu aliyozaliwa Harmonize au Harmo, walisikika wakimuomba agombee ubunge kwenye Jimbo la Tandahimba. Baadhi ya wanakijiji hao walikaririwa wakisema; “Raj (Harmonize) ni kijana wetu, ni mtoto wa hapa Mahuta, kiukweli ametupa heshima kubwa mno sehemu mbalimbali nje na ndani ya Tanzania.
“Amesababisha hata watu kujua kuna Kijiji cha Mahuta, tunamuomba agombee hata ubunge tunaamini atatuwakilisha vizuri na kutusemea shida zetu za hapa kijijini. “Na sisi tunatamani maisha mazuri hivyo Raj akija kugombea tutampa ubunge bila shida yoyote.”
Hata hivyo, Harmo hakuwapa majibu ya kueleweka hivyo Gazeti la Ijumaa Wikienda lilimtafuta Harmo ambaye alifunguka juu ya ishu hiyo ambayo imeibuka tena hivi karibuni baada ya kuachia wimbo wake wa Magufuli. Harmo alisema hajapokea maombi hayo rasmi, lakini ndoto yake kubwa kwa sasa ni kuwekeza kwenye muziki wake kuhakikisha unafika mbali na kwenye levo za juu za kimataifa.
“Ndoto yangu kubwa ni kuwekeza sana kwenye muziki wangu ili ufike mbali na kwenye levo za kimataifa. “Huko ndiko ninakoweka nguvu kubwa sana kwa sasa. Kwa hiyo chochote ninachokifanya ni kwa ajili ya kukuza muziki wangu.
“Kifupi sifikirii kabisa kujiingiza kwenye siasa badala yake ninafikiria zaidi kuupeleka huu muziki wetu mbali sana ili uweze kuwa mkubwa zaidi,” alisema Harmo ambaye kwa sasa anafanya vizuri kupitia nyimbo zake mbalimbali kama Never Give Up, Magufuli, Kainama, Niteke na nyingine kibao.
Harmo alitinga jijini Dar mwaka 2009 alipohitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mkundi mkoani Mtwara. Baada ya kuwasili jijini Dar, hakuwa na shughuli ya kufanya hivyo alijikita katika uuzaji wa chai maeneo ya Kariakoo.
Baadaye Harmonize alijihusisha na biashara ya nguo na vitu mbalimbali. Alianza harakati za muziki mwaka 2011 akirekodi kwenye studio mbalimbali, lakini nyimbo zake hazikuwa na ubora wa kupelekwa katika vituo vya redio hadi alipokutana na Diamond au Mondi kwenye Ukumbi wa Dar Live ambapo alimchukua kwenye Lebo ya Wasafi na ndiyo ukawa mwanzo wa kung’aa hadi leo.