Esma Afichua Mpango Mimba ya Tanasha Kuharibika
WAKATI akiwa amebakiza mwezi mmoja wa kujifungua, dada wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Esma Khan ‘Esma Platnumz’ amefichua mpango wa mimba ya wifi yake, Tanasha Donna kuharibiwa.

Tanasha ambaye pia ni mtangazaji wa Redio ya NRG ya jijini Mombasa, Kenya, kwa sasa ana mimba ya miezi nane aliyopewa na Diamond au Mondi.


Akizungumza na Gazeti la Ijumaa, Esma alifichua mpango wa mimba hiyo kuwa kuna watu wanaojifanya wana uhusiano wa kimapenzi na Diamond huku wengine wakitumia njia mbalimbali za kumchanganya akili Tanasha kwa lengo la kumharibia mimba yake.

“Tanasha wala hana muda wa kusikiliza mambo ya mtandao au nini wanachosema kuhusiana na maisha yake na mpenzi wake. Ujue kuna watu wanafanya hivi makusudi wakiamini Tanasha akiingia mitandaoni atashtuka au atachanganyikiwa.


“Ninachoshukuru mimi Tanasha hana mambo ya Kiswahili kabisa wala muda wa kuangalia nini kimepostiwa mtandaoni kwa sababu anajua watu wengi wanazungumza tu wala hawajui maisha ya kweli ya mtu binafsi,” alisema Esma.


Dada wa mwanamuziki huyo alizidi kutiririka kuwa anajua watu wengi wanapenda kuleta machafuko kwenye kipindi alichonacho Tanasha wakiamini kabisa mimba itaharibika.


“Kwa taarifa yao tu, kama ndugu, Tanasha amebakiza mwezi mmoja hivyo tumejiandaa kumpokea mtoto, hayo maneno mengine wala hatuwezi kuyasikiliza au kutuchanganya,” alimaliza kusema Esma.