Erick Kabendera Asomewa Mashtaka Mahakamani
MWANDISHI wa habari Tanzania Erick Kabendera leo, Agosti 5, 2019, amepandishwa kizimbani kusomewa mashtaka mapya ya kosa la kimtandao baada ya lile la idara ya Uhamiaji kujiridhisha juu ya uraia wake.

Amefunguliwa mashtaka mapya ya kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu na uchumi nchini na kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya Sh. milioni mia moja za Kitanzania.  Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya Sh. millioni mia moja na sabini.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliyowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyafanya makosa hayo kati ya Januari 2015 na Julai mwaka huu jijini Dar es Salaam na baadhi ya makosa hayo anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano na watu ambao hawakuwepo mahakamani leo.

Makosa yote hayana dhamana. Mawakili wake wameondoa ombi la dhamana kutokana na mashtaka hayo mapya. Akizungumza na wanadishi wa habari punde baada ya Kabendera kusomewa mashtaka, wakili wake Jebra Kambole amesema:

“Wakati Erick anakamatwa siku ya kwanza aliambiwa kosa lake ni la uhamiaji, akapelekwa kwenye mamlaka za uhamiaji, akahojiwa, pasipoti yake ikachukuliwa. Uhamiaji wakamkabidhi kwa jeshi la polisi makao makuu (central) ya  Jeshi la Polisi wakamhoji kwa makosa ya uchochezi.  uanzia hapo hajawahi kuhojiwa kwa makosa mengine zaidi ya hayo.”

Amefafanuwa kwamba kutokana na kwamba mashtaka aliyosomewa Kabendera hayana dhamana, ameshindwa kutoka leo.

“Tunachofanya sasa, ni kuangalia upelelezi unafanyika kwa wakati,” ameeleza wakili huyo. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa Agosti 19 mwaka huu.

Kabendera anayeandikia magazeti ndani na nje ya Tanzania, alikamatwa Jumatatu, Julai 29, wiki iliyopita na watu waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi. Katika mkutano na vyombo vya habari, kamanda wa polisi kanda maalum ya mji wa Dar,  Lazaro Mambossasa,  amesema kuwa mshukiwa huyo alikaidi agizo la polisi la kufika mbele yao kwa ajili ya mahojiano.

”Mwandishi huyu aliitwa, hakutekwa lakini kwa ujeuri alikaidi wito huo… Kimsingi pengine iwapo angewasili angehojiwa na kuachiliwa,”  alisema Mambossasa