DC Aagiza Wachimbaji Madini Kukamatwa
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mtemi Msafiri, ameamuru kukamatwa kwa wachimbaji wakubwa wa madini katika eneo la Matabe wilayani humo, ambao wanadaiwa kuwa wasumbufu kwa wachimbaji wadogo wa madini katika eneo hilo.


Mkuu wa Wilaya Mtemi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wachimbaji  wadogo zaidi 1000, katika eneo la Matabe, kikao ambacho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Constantine Kanyasu, ambapo amesema licha ya maamuzi hayo wachimbaji hao wafuate sheria.

Maamuzi hayo yamekuja kufuatia malalamiko mengi kutoka wachimbaji wadogo kuwalalamikia wachimbaji wakubwa.

"Malalamiko haya yanayotokea kwa wachimbaji hawa wadogo, sisi kama Serikali hatukubali kuyavumilia, OCD nakuagiza hakikisha wachimbaji wakubwa unawakamata na wanachukuliwa hatua za kisheria", amesema Mkuu wa Wilaya Mtemi.

Awali Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kupitia Menejimenti ya Shamba la Miti la Biharamulo mkoani Geita, idhibiti upanuzi wa uchimbaji madini unaofanywa na wachimbaji wadogo nje ya yale ambayo yanatambulika kwa shughuli hiyo katika Shamba hilo.