Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya na Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwashawishi Wataalamu wake kujifunza fani tofauti ili kuziba mapengo alipofika kufanya ziara ya kukagua Vitengo tofauti vya Hospitali ya Mnazo Mmoja.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Maabara katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Msafari Marijani akimuelezeas Balozi Seif changamoto wanazopambana nazo Watendaji wake katika kutoa huduma kwa Wananchi.
Mkuu wa Kitengo cha Kuhudumia Wagonjwa mahututi {ICU} Dr. Salum Shaaban Salum akimpatia maelezo Balozi Seif huduma zinazotolewa katika Kitengo hicho kinachohitaji utulivu wa hali ya juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Ali Salum Ali akifafanua mpango wa Wizara ya Afya wa kutafuta suluhisho la kudumu la upatikanaji wa Gesi ya Oxgen kwa ajili ya Hospitali za Serikali. Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar kuendelea kuwashawishi Wataalamu wake wa Afya kusomea fani nyengine zenye upungufu wa watendaji ili kuziba mapengo yanayojitokeza katika utoaji wa huduma za Afya.
Alisema lazima ifikie wakati Hospitali za Serikali ziwe na uwezo kamili wa kuwa na Wataalamu wa kutosha badala ya kuendelea kutumia mfumo wa muda mrefu uliozoeleka wa kutegemea Wataalamu wa Nje.
Akifanya ziara fupi ya kukagua uwajibikaji kwa Watendaji tofauti kwenye Vitengo mbali mbali vinavyotoa huduma za Afya kwa Wananchi ndani ya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Balozi Seif Ali Iddi alisema hatua hiyo ya ushawishi inaweza pia kusaidia kuziba mapengo ya Wataalamu wanaostaafu kwenye Vitengo vya Fani hizo.
Balozi Seif alikitolea mfano Kitengo kinachohudumia Wananchi wanaopatwa na ajali  ambacho kinastahiki kuimarishwa zaidi kwa vifaa pamoja na Wataalamu wazalendo waliobobea kwa vile ajali za vyombo vya Moto hivi sasa zimeongezeka mara dufu bara barani kutokana na harakati za Kimaisha.
Alisema takwimu inaonyesha wazi kwamba Wagonjwa wengi wanaopelekwa Hospitali kwa ajili ya huduma za Afya ni wale wanaopatwa na ajali za bara barani ambao wengi kati yao hulazimika kupelekwa nje ya Zanzibar baada ya kesi zao zinazohusiana na mifupa kushindwa kuhudumiwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba lazima Taasisi za Umma zijitegemee kwa kuwa na Wataalamu pamoja na Vifaa vya kutosha ili kuepuka tatizo la kuwapeleka wagonjwa nje Zanzibar sambamba na kuacha kusubiri Wataalamu wa misaada.
Alifahamisha kwamba upatikanaji wa huduma za uhakika katika Vituo na Hospitali za Umma ndio njia pekee itakayojenga imani na upendo kwa Watendaji wa Sekta hiyo kutoka kwa Wananchi walio wengi Nchini.
Mapema Mkurugenzi wa Kitengo cha Maabara katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Msafari Marijani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uwezo wa kutoa huduma kwa saa 24 kwenye Kitengo hicho bado haujakamilika kutokana na uhaba wa Wataalamu wa Fani hiyo inayohitaji kufanyiwa kazi ya kuwahamaisha Watendaji wake kuzidi kupata mafunzo zaidi ili kujaza pengo liliopo.
Dr. Marijan alisema Kitengo hicho hutoa huduma kuanzia asubuhi hadi majira ya Saa Tatu za Usiku kwa sasa. Lakini hata hivyo Watendaji wake hulazimika kuwajibika katika muda wa ziada pale inapotokea kesi ya dharura inayohitaji kufanyiwa kazi ili kunusuru maisha ya Mgonjwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Ali Salum Ali alisema Wizara ya Afya kupitia Uongozi wa Hospitali hiyo ina mpango  wa kuimarisha Miundombinu Mipya katika Hospitali hiyo  tegemezi kwa Wananchi walio wengi Kisiwani Unguja.
Dr. Ali alisema Majengo mengi ya Hospitali hiyo ni ya zamani yakiwa yameshapitwa na wakati ambayo  yanahitaji kufanyia matengenezo makubwa vikiwemo baadhi ya vifaa kwenye Vitengo tofauti.
Akizungumzia changamoto inayojitokeza ya Hewa ya {Oxgen} kwenye Hospitali ya Mnazi Mmoja Dr. Ali alisema Timu ya Wizara ya Afya hivi sasa iko Jijini Dar es salaam kufanya mpango wa utafiti wa upatikanaji wa mfumo mwengine wa Liquid Oxgen badala ya ule uliozoeleka ambao hukumbwa na matatizo ya mara kwa mara.
Alisema mtambo wa kutengeneza hewa ya Oxgen uliopo Mnazi Mmoja uliopatikana kwa msaada wa ufadhili Kutoka Nchini Uturuki Mnamo Mwaka 2017 hivi sasa umeharibika na unafanyiwa matengenezo ili ubakie kuwa wa hakiba.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja alifahamisha kwamba Wizara ya Afya imejipanga kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa hewa safi ya Oxgen linalozikumba takriban Hospitali zote Nchini katika kipindi cha Miaka 20 sasa.
Alisema Mpango huo umelenga kujengwa kwa Mtambo Mkubwa wa kuzalisha Oxgen katika kiwango cha Mitungi yenye ujazo wa Lita 10,000 utakaowezesha kusambazwa kwa Taasisi nyengine Nchini zitakazohitaji hewa hiyo katika matumizi yao ya kawaida.
Alieleza kwamba kiwango hicho kitakachozalishwa kwenye Mtambo Mpya huo utakaojengwa kinatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na hakiba ya hewa ya Oxgen kwa asilimia 25% ya ziada.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada ilizochukuwa za kusaidia upatikanaji wa Hewa ya Oxgen kwa Hospitali za Serikali ambapo kwa sasa mahitaji halizi ni Mitungi 43 kwa Siku.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar