Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo amesema asilimia kubwa ya madaktari walioko nchini wana msongo wa mawazo kutokana na kazi kubwa ya kuhudumia watu waliyonayo.


Waziri Jafo ameyabainisha hayo leo Agosti 20 alipokuwa akizungumza na Waganga Wakuu wa Mikoa katika mkutano wao mkuu wa tatu uliofanyika mkoani Dodoma, ambapo amewapongeza kwa kazi yao kubwa, kwani wamekuwa wakijituma na kuwa mstari wa mbele kuokoa maisha ya watanzania.

''Niwapongeze madaktari wa Tanzania kwa kazi kubwa mnayoifanya, hili naomba nilisisitize nazungumza kwa dhati ya moyo wangu,  madaktari wetu mnafanya kazi kubwa sana ya dhati iliyopitiliza na mimi wakati wote nikiona mtu anabeza kazi ya madaktari huwa napata huzuni sana", amesema Jafo.

"Nimefika nilikuwa nawaangalia, wengi sana naona mna 'stress', mkutano umepooza,  ninachoamini kwamba wengi mnastress lakini stress hizo ni kwa kazi kubwa mnazofanya'' ameongeza Waziri Jafo.

Aidha katika pongezi zake  Waziri Jafo, ameeleza ni kwa namna gani aliwaona wakijitoa kuhudumia majeruhi wa ajali ya kulipuka kwa tenki la mafuta mkoani Morogoro.

''Mfano mzuri ni wa tukio kubwa la tenki la mafuta kuwaka moto Morogoro,nimefika pale mpaka saa tano za usiku, niliwaona madaktari hata mioyo
imeshakufa ganzi, watu waliokuwa katika hali mbaya, madaktari wakijituma kuwasindikiza Muhimbili".