Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE, John Myola akizungumza kwenye kikao cha kuhitimisha Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana katika kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE, John Myola,akizungumza kwenye kikao hicho na kuwataka viongozi wa kata ya Usanda, mtendaji wa kata, maendeleo, viongozi wa dini, kimila,vitongoji na waelimishaji rika, na kuwataka waendeleze mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia zikiwamo mimba na ndoa za utotoni, licha AGAPE kusitisha mradi wao kwenye kata hiyo.

Prosper Ndaiga kutoka Shirika la AGAPE akimwakilisha Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana katika kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Lucy Maganga ,akielezea namna mradi huo ulivyofanya kazi kwenye kata hiyo ya Usanda na hatimaye kupunguza matukio ya ukatili zikiwamo mimba na ndoa za utotoni.

Mtendaji wa kata ya Usanda Emmanuel Maduhu, akipongeza Shirika la Agape kwa kupeleka Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana, ambao umesaidia kupunguza matukio ya ukatili zikiwamo mimba na ndoa za utotoni.

Afisa Maendeleo kata ya Usanda Halima Tendega, akielezea Shirika hilo la AGAPE namna lilivyosaidia kupunguza matukio ya ukatili zikiwamo mimba na ndoa za utotoni tofauti na hapo awali hali ilikuwa mbaya.

Mratibu Elimu kata ya Usanda Sospeter Kasonta, akipongeza Shirika la AGAPE kwa kupunguza matukio ya ukatili, ukiwemo utoro mashuleni, mimba na ndoa za utotoni, huku akitoa na ushahidi kwa takwimu, ambapo mwaka 2016 kulikuwa na mimba 21, (2017) 16, )2018) nne na )2019) mimba moja.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Manyada Daudi Michael, akielezea namna Shirika la Agape lilivyosaidia kuifumbua jamii juu ya matukio ya ukatili na kupinga mimba na ndoa za utotoni, ambapo wao wameshapiga marufuku wanafunzi kucheza shoo kwenye maharusi.

Geofrey Maganga ambaye ni muelimishaji rika kutoka kitongoji cha Mwagala, naye akielezea namna jamii ilivyobadilika mara baada ya kupata elimu kutoka kwenye Shirika la Agape, na kuanza kusomesha watoto wao hasa wa kike.

Mzee wa kimila Shija Kulwa, akielezea namna Shirika hilo la Agape lilivyosadia kubadili mitazamo jamii na kuachana na masuala ya mila na desturi kandamizi ambazo zilikuwa zikisababisha kuendelea kuwepo masuala ya ukatili ndani ya jamii pamoja na kuozesha watoto ndoa za utotoni.

Muelimishaji rika kutoka kitongoji cha Mwagala Mary John akielezea namna jamii ilivyobadilika mara baada ya kupewa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape.

Mchungaji kutoka Kanisa la AICT Usanda Lameck Makungu, akielezea namna Shirika la Agape lilivyosaidia kuikoa jamii, ambapo wao kama viongozi wa kidini walipokuwa wakipinga matukio hayo ya ndani ya jamii, waumini walikuwa wakihama madhehebu kwa sababu ya kugusa maslahi yao.


Viongozi kutoka kata ya Usanda, wakiwemo wa vitongoji, afisa maendeleo, mtendaji, mratibu elimu pamoja na viongozi wa kidini, kimila, na waelimishaji rika, wakiwa kwenye kikao cha Shirika la Agape cha kuhitimisha mradi wao wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwenye kaya hiyo. Picha zote naa Marco Maduhu- Malunde 1 Blog.

Shirika lisilo la kiserikali la AGAPE AIDS CONTROL PROGRAM la Mkoani Shinyanga, limehitimisha Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana ambao ulikuwa unatekelezwa katika kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambao ulilenga kutokomeza masuala ya ukatili wa kijinsia zikiwemo mimba na ndoa za utotoni.

Kikao cha kuhitimisha mradi huo wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana, kimefanyika leo Agosti 2,2019 katika shule ya Msingi Shingita iliyopo kwenye kata ya Usanda, na kuhudhuriwa na mtendaji wa kata, mratibu elimu kata, Afisa maendeleo, wenyeviti wa vitongoji, viongozi wa kidini, wazee wa kimila, pamoja na waelemishaji rika.

Utekelezaji wa mradi huo wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia ulianza mwaka (2017) na kuhitimishwa June 30 mwaka huu (2019), ambapo Shirika la AGAPE lilikuwa likiutekeleza kwenye kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Sida la nchini Sweden kupitia Save the Children.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mradi huo,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE, John Myola ,amewaasa viongozi wote wa kata hiyo ya Usanda,wakiwemo wazee wa kimila na waelemishaji rika, kuyaendeleza mapambano ya kupinga ukatili ndani ya jamii zikiwemo mimba na ndoa za utotoni.

Amesema licha ya AGAPE kuhitimisha mradi huo kwa awamu ya kwanza isiwe ndiyo mwisho wa kuendeleza mapambano ya kupinga ukatili pamoja na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, ambapo kila mtu anapaswa awajibike kwa nafasi yake ikiwemo na viongozi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano mbalimbali na kutomeza matukio hayo.

“Sisi AGAPE leo tumekuja kuhitimisha rasmi mradi wetu wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kwenye kata hii ya Usanda, ambao ulilenga kutokomeza masuala ya ukatili wa kijinsia, zikiwamo mimba na ndoa za utotoni,”amesema Myola.


“Hivyo kutokana na sisi kuhitimisha mradi wetu huu, tunaomba na nyie sasa viongozi wa Kata hii ya usanda mkiwemo viongozi wa kidini,wazee wa kimila, wenyeviti wa vitongoji na waelimishaji rika, muendeleze mapambano haya ili msirudi kule mlikotoka, ambapo awali kata hii ilikuwa ikiongoza kwa mimba na ndoa za utotoni,”ameongeza Myola.


Pia amewataka wazazi na walezi kwenye kata hiyo , wawekeze watoto wao kwenye elimu na kuacha kuthamini mifugo, na kuozesha watoto wao ndoa za utotoni, ambapo pindi watakapohitimu masomo yao na kupata kazi nzuri, watakuja kuwasaidia baadae, pamoja na kuwanunulia hiyo mifugo ambayo wanaitaka.

Naye mtendaji wa kata ya Usanda Emmanuel Maduhu, amelipongeza Shirika hilo la AGAPE kwa kupeleka mradi huo katani humo, ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia zikiwamo mimba na ndoa za utotoni.

Kwa upande wake mratibu elimu kata ya Usanda Sospeter Kasonta, amesema Shirika hilo la Agape limesaidia kupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi, ambapo mwaka (2016) kulikuwa na mimba 21, (2017) 16, (2018) mimba nne (4), na mwaka huu mpaka sasa kuna mimba moja tu ya sekondari.