Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka wananchi nchini wawe na utamaduni wa kushirikiana na Serikali kujenga shule, zahanati, vituo vya polisi katika maeneo wanayoishi kuliko kuwa na akili potofu miradi hiyo inajengwa na Serikali pekee.

Lugola ameyasema hayo wakati akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni kwake Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo pia alishirikiana na wananchi wa Kijiji cha Namalebe kushiriki ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Ibwagulilo iliyopo katika Kata ya Chitengule jimboni humo ambayo Serikali imetenga shilingi milioni 96 kwa ajili ya kuikamilisha shule hiyo.

“Mradi huu unaendelea vizuri, ambapo Serikali imetupa milioni 96.9 kuukamilisha mradi huu, nami nipo hapa na nimeshirikiana na wananchi wangu kujitolea kujenga shule hii ambayo itawasaidia wananchi wa Kata hii ili Watoto wao waweze kupata elimu,” alisema Lugola.

Waziri Lugola pia aliwahamasisha wananchi hao kushiriki matukio ya maendeleo, pia alitoa mabati, saruji, nondo kwa ajili ya ujenzi wa zanahati, na kuongeza madarasa katika shule mbalimbali zilizopo katika jimbo lake.
Naye Fundi Mkuu wa Shule ya Msingi, Marco Malima, alimshukuru Waziri huyo kwa kufika katika eneo la ujenzi huo na imewapa nguvu zaidi kufanikisha ujenzi huo kwa wakati.

“Fedha na vifaa kukamilisha ujenzi huu zipo, ujenzi huu ulianza mwezi mei mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi wa saba mwaka huu, ambapo tunajenga madarasa, nyumba za walimu pamoja na vyoo,” alisema Malima.
Waziri Lugola anaendelea na ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo jimboni humo pamoja na kuzungumza na wananchi na kutatua kero zao zinazowakabili.

Lugola amewataka wananchi wa jimbo lake, waendelee kumuamini na kushirikiana naye wakati wanahakikisha jimbo hilo linakua jipya zaidi kimaendeleo.
 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, leo. Lugola amewataka wananchi nchini wawe na utamaduni wa kushirikiana na Serikali kujenga shule, zahanati, vituo vya polisi katika maeneo wanayoishi kuliko kuwa na akili potofu miradi hiyo inajengwa na Serikali pekee. 
 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akibeba tofali kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Ibwagulilo, ikiwa ni kuwahamasisha wananchi wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo mpya. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akikagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Ibwagulilo, iliyopo Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara. Lugola amewataka wananchi nchini wawe na utamaduni wa kushirikiana na Serikali kujenga shule, zahanati, vituo vya polisi katika maeneo wanayoishi kuliko kuwa na akili potofu miradi hiyo inajengwa na Serikali pekee. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.