Viongozi watatu wa kikundi cha wachimbaji dhahabu wadogo cha Winima Group kilichopo katika mgodi wa dhababu Kitunda Wilayani Sikonge Mkoani Tabora  wanatarajia kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutafuna shilingi mililioni 342 za mauzo ya kilo 1.549 za dhahabu.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Tabora jana, kwa niaba ya wachimbaji wenzake, Shabani Seifu amesema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya wachimbaji hao kukaa kikao jumatatu Julai 1, na baadhi ya viongozi.

Amesema kuwa Machi 27 mwaka huu watuhumiwa hao walikwenda wilayani Nzega kwa ajili ya kufanya mauzo ya kilo 1.5 za dhahabu zikiwa ni mali ya wanakikundi hao lakini baada ya kuuza dhahabu hiyo walirudi wilayani Sikonge lakini hawakukabidhi mauzo hayo.

Amewataja viongozi wanaotuhumiwa kuwa ni Mwenyekiti wa kikundi hichoJaphet Mbwilo, Katibu wa kikundi Godfrey Mwaniwiti na Meneja wao Bazilio Bazilio.

Seif amedai baada ya kuuza dhahabu hiyo na kukabidhiwa kitita chote hawakuchukua askari wa kuwasindikiza ila waliamua kununua gari aina ya PRADO yenye namba za usajili T 294 BER kwa sh mil 10 wakati waliafikiana kuchukua askari polisi kwa ajili ya ulinzi na posho yao iwe sh mil 5.

Wanakikundi hao walimwomba Waziri wa Madini Doto Biteko aingilie kati ili waweze kupata haki yao pia wameliomba jeshi la polisi lisaidie kukamatwa wahusika na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Naye Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa ACP Emmanuel Nley amesema kuwa wamepata taarifa za tukio hilo na uchunguzi umeanza ili kubaini ukweli uko wapi.