Mahakama ya Hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, leo Julai 26, 2019, imewahukumu miaka 20 jela kila mmoja washtakiwa wanne kwa kosa la uhujumu uchumi.

Kesi hiyo namba 55 ya mwaka 2018, imetolewa hukumu na Hakimu Ismael Ngaile, ambapo inaelezwa washtakiwa hao walikamatwa mwaka 2018, katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kukutwa na nyama ya Pundamilia pamoja na miguu ya mnyama huyo.

Watuhumiwa hao James Mwita na Yohana Mahende,  wakazi wa Kisangura walikutwa na nyama hiyo yenye thamani ya shilingi 2,616,000,  huku wenzao Athuman Zakaria na Juma Chacha walikutwa na miguu ya mnyama huyo.