Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi katika kuhakikisha wananchi mkoani humu wanakuwa na vyoo imara na bora, amewashukia wanaume ambao nyumba zao hazina vyoo kwa kusema hawana sifa ya kuitwa wanaume mashine.

Zambi aliyasema hayo jana, alipozungumza na wananchi wa kata ya Nachingwea, manispaa ya Lindi.

Alisema baadhi ya nyumba hazina vyoo, na nyingine zinavyoo visivyoridhisha na vinatia aibu. Ingawa wenye nyumba hizo, hasa wanaume wanajiona wanasifa zinazoweza kuwafanya wajiite mashine.

''Mnasema mwanaume mashine, mashine gani wakati anashindwa kujenga choo!,'' alihoji Zambi. 5: Alisema sifa ya mwanaume anayestahili kujiona ni mashine ni yule ambaye nyumba yake ina choo. Sio anae vizia choo vya jirani zake wakati ana mke na watoto.

Alibainisha kwamba muda wa kuwa na choo vinavyotia aibu umekwisha. Kwahiyo wananchi mkoani humu, ambao hawana choo imara na bora wajenge kabla ya kuanza ukaguzi wa nyumba kwa nyumba.

Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa mkoa wa Lindi amewaagiza watendaji wa mitaa na vijiji vilivyopo mkoani humu, wasimamie kikamilifu kampeni ya nyumba ni choo, ili nyumba zote ziwe na choo imara na bora.