Msanii wa muziki, Diamond Platnumz amesema haamini kuwa uhaba wa Kondomu za kike ni chanzo cha maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kwakuwa sio wote wawili wanaotakiwa kuvaa bali akivaa mmoja inatosha.

Ametoa kauli hiyo, alipokua akizungumza na waandishi wa habari katika baada ya kutangaza kushirikiana na Tume yaKudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), katika kutoa elimu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi ambapo amesema wanaume ndio wanaowadanganya wanawake kuhusu matumizi ya kinga.

“Siamini kwamba kutopatikana kwa Kondomu za kike kunachangia maambukizi kwasababu sio lazima wavae wote wawili hivyo akivaa mmoja inatosha ni jambo la kueleweshana tu,” amesema.

“Sisi wanaume ndio tunaoongoza kulazimisha mtu asivae kinga sasa dada zangu mjiulize ni kwanini mtu afanye hivyo, maana yake hana nia nzuri na wewe itakua anataka upate ujauzito kwa lazima au nia nyingine mbaya na anakufanyia makusudi, ninaamini wanawake wakitusaidia kuweka misimamo kuwa haiwezekani basi haitawezekana,” amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Tacaids, Jumanne Issango amesema kuna changamoto za upatikanaji wa Kondomu za kike na kuwataka vijana kutotumia nafasi hiyo kama sababu ya kutokuelewa na kutumia elimu zinazotolewa.