Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel akizungumza na Wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanaosoma katika Sekondari ya Longido
Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel akiwa na Wanafunzi 41 wenye ulemavu wanaosoma katika shule ya Sekondari Longido
Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel akikabidhi moja kati ya zawadi alizojaaliwa kuzipeleka katika shule ya Msingi Longido
Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel akiwa na Mwanafunzi Mwenye ulemavu wa ngozi Ummy ambaye aliwakilisha mkoa wa Arusha katika mashindano ya Umiseta Mtwara katika Riadha na hatimaye kuuletea mkoa medali ya dhahabu.

Wanafunzi wenye ulemavu wameshauriwa kuzingatia masomo na kusoma kwa bidii ili kujiandalia maisha yao ya baadae kwa kuwa elimu ndio mtaji wa maisha yao.

Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel alipotembelea shule ya Sekondari Longido pamoja na shule ya msingi Longido wilayani Longido katika mkoa wa Arusha, ambazo zote zina vitengo Maalum kwa ajili ya watoto wenye Ulemavu.

Akizungumza na wanafunzi hao, Amina ametoa ushuhuda kuwa safari yake ya maisha pamoja na kuwa na vikwazo vingi hadi kufika alipo sasa ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu pamoja na kusoma kwake kwa bidii elimu ambayo imemsaidia kumpa mwanga katika maisha yake.

Amewataka wanafunzi hao kutokujiona wapweke kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano inawapenda na kuwajali na ndio maana Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza hapa nchini tangu kupata uhuru amewateua watu wenye ulemavu kumsaidia kwenye serikali yake pasipo kujali ulemavu walionao.

Akiwa katika shule ya Msingi Longido, Amina amewashuhudia watoto wasioona ambao baadhi yao hutelekezwa na wazazi wao wanapowafikisha shuleni hapo.

Mbunge huyo amewaomba wasamaria wema kujitoa katika kuwasaidia watoto wenye uhitaji kwa kuwapatia mahitaji muhimu kama nguo, mafuta, sabuni pamoja na mahitaji mengine muhimu yatakayowasaidia kutimiza malengo yao.

Ameipongeza shule ya Sekondari Longido kwa matokeo mazuri ya kidato cha sita waliyopata kwa mwaka huu ambapo wanafunzi wengi wamefaulu daraja la kwanza na lile la pili. 

Amina Ametoa zawadi ya Computer moja, counter book pamoja na sabuni na mafuta kwa shule ya Sekondari Longido.

Katika ziara hii aliongozana na viongozi wa Uwt pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi.