Serikali imewataka wajane kote Nchini kukumbuka kuhusu suala la VVU/UKIMWI na kuwataka kuchukua tahadhari kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI kwa kutumia kinga, kuepuka tabia hatarishi, kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

Akiongea wakati wa kufungua Mafunzo ya kujenga uwezo kwa wajane Mkurugenzi Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii  Mwajuma Magwiza alisema kuwa UKIMWI hadi sasa bado ni janga la Kitaifa hivyo kusisitiza wajane hao kuchukua tahadhari kubwa ili kuepukana maambukizi.

Aidha  Magwiza pamoja na kuzungumzia maambukizi ya UKIMWI lakini pia amesema tayari serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuhamasisha jamii kuacha Mila na Desturi potofu za kunyanganya mali za wajane, kuozesha watoto wakike katika umri mdogo ikiwemo kutakasa na kurithi wajane.

Bi. Magwiza ameitaka jamii pia kuachana na mila zenye madhara kwa mwanamke hususan mjane na zinazodhoofisha jitihada zake za kujikwamua kifikra, kiutamaduni, kiuchumi na kijamii akiongeza kuwa kila mmoja anao wajibu wa kutoa fursa sawa kwa makundi yote katika jamii ikiwemo wajane kubadili fikra, mtizamo, kuwa jasiri, kujiamini na kutambua kuwa mabadiliko yanaanza na wao.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bi. Mboni Mugaza amewambia wajumbe wa Mafunzo hayo kuwa lengo la Wizara yake ni kuwakutanisha wadau na viongozi wadini ili waweze kujua huduma zinazotolewa na wajane lakini pia kuwajengea uwezo ili waweze kukabiliana na changamoto za kimaisha ukizingatia kuwa wengi wao ni wakuu wa familia.

Bi. Mariamu Aswile ambaye pia ni Mratibu wa Umoja wa Wajane Kanda ya Mashariki akizungumza na vyombo vya habari kuhusiana na mafunzo hayo amesema wosia ni jambo la Msingi kwa kulinda haki za wajane lakini pia akasisitiza suala la mjane kupewa hati ya kifo ili iwe hatua muhimu ya mjane husika kufuatilia mirathi itakayomsaidia kusaidia wazee.

Aidha Bi. Aswile amewata wananchi kufuatilia zaidi madhira na madhara wayapatayo wajane ili na wao wasije yakawakuta matatizo ambayo yanawakabili wajane kwa sasa kwani kila mmoja ni mjane mtarajiwa hivyo ni muhimu kwa wajane watarajiwa na wapya kuhakikisha wanachukua tahadhari kuepukena na madhara na changamoto za wajane walizonazo sasa.

Wakati huohuo Mjane Bi. Stella Maveka kutoka kikundi cha Wajane Tuinuane kilichopo mjini Dodoma ameyataja mafunzo hayo kuwa ya muhimu kwa wajane kwani yatawasaidia wajane kujua taratibu za usajili wa vikundi na wakati huo akilaani baadhi ya vyombo vya dora vinavyokamata biashara za wajane na kuitaka serikali kuchukua hatua ili kuokoa bidhaa hizo ambazo zinazuiliwa na mamlaka za serikali.

Mafunzo haya yanafanyika kufuatia agizo la Naibu Waziri Afya Dkt. Faustine Ndugululile alilolitoa katika Kongamano la Wajane mapema mwezi Juni Mwaka huu kwa Wizara yake kutaka Wajane wapatiwe mafunzo ya ujasiliamali na vifungashio lakini pia namna bora ya kumiliki ardhi na kwa wajane kupatiwa huduma ya Afya.

Utafiti uanaonesha kuwa kati ya 7% hadi 16% ya wanawake wote duniani bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kupoteza haki ya kumiliki mali , umasikini , mila na desturi za kuridhiwa baada yakufiwa uku idadi ya wajane Tanzania ambao ni wa wanachama wa TAWIA(Tanzania Widows Association) ikifikia 800,000.
 Mkurugenzi Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Mwajuma Magwiza akiongea wakati wa kufungua Mafunzo ya kujenga uwezo kwa wajane yaliyofanyika leo Jijini Dodoma.
 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Mboni Mgaza akielezea malengo ya mafunzo wakati wa Mafunzo ya kujenga uwezo kwa wajane yaliyofanyika leo Jijini Dodoma.
 Mkurugenzi Idara ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Julius Mbilinyi akioelezea umuhimu wa kumuwezesha mjane kiuchumi wakati wa Mafunzo ya kujenga uwezo kwa wajane mafunzo yaliyofanyika leo Jijini Dodoma.
 Mratibu wa Chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) Kanda ya Mashariki Mariamu Aswile akitoa shukrani kwa niaba ya wajane wakati wa kufungua Mafunzo ya kujenga uwezo kwa wajane yaliyofanyika leo Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajane wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na maafisa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mara baada ya ufunguzi wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo leo Jijini Dodoma. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW