Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewataka ndugu wa maaskari waliofariki wasiwe chanzo cha machungu kwa wake za marehemu, kwa kutaka kujimilikisha mali walizoachwa.

IGP Sirro amesema hayo Julai 27, wakati wa kuaga miili ya askari polisi watatu waliofariki katika ajali ya gari, iliyotokea Julai 25 baada ya gurudumu la nyuma kupasuka na kupinduka, wakati wakitekeleza majukumu yao ya kikazi maeneo ya Mkuranga mkoani Pwani.

”Wakati mwingine tunapoondoka sisi wakuu wa familia, kuna baadhi ya watu kwenye familia wanakuwa tatizo,  kama baba aliacha nyumba wale tegemezi wanaingilia mambo ya nyumba, tuache wenzetu wamepata msiba mkubwa, tuache ile mali iliyotafutwa na wenzi wao isaidie watoto wake na familia, tusiwe watu wakuongeza machungu zaidi,  tusiwe  vikwazo”. Amesema IGP Sirro.

Aidha IGP Sirro amesema, Jeshi la Polisi litahakikisha stahiki zote za marehemu zinapatikana kwa muda muafaka ili ziweze kusaidia familia zao.

Waliofariki katika ajali hiyo ni ACP Issah Bukuku, Inspekta Esteria wa Ofisi ya RCO Rufiji pamoja na PC Lameck wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Ghasia Rufiji.