Kamishina wa Uraia na Pasipoti kutoka Idara ya Uhamiaji Gerald Kihinga.

IDARA ya Uhamiaji imesema inamshikilia Mwandishi Erick Kabendera na kwa sasa wanaendelea kuchukua taarifa zake kuhusu uhalali wa uraia wake.

Kamishina wa Uraia na Pasipoti kutoka Idara ya Uhamiaji Gerald Kihinga amesema wanamshikilia Kabendera ili kujiridhisha na uraia wake na huo ni wajibu wao pale wanapokuwa na mashaka na uraia wa mtu.

"Idara ya Uhamiaji ilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusiana na utata wa uraia wa Erick Kabendera mwenyewe alikua hajawahi kuhojiwa kuhusiana na uraia wake, kwa kuwa hakufika ofisini pamoja na kumtumia wito mara kadhaa wa kumtaka afike ofisini kwa mahojiano.

"Na ndio maana sasa idara ya uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imeweza kumtafuta na kumkamata mhusika ili aweze kuhojiwa kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi kuhusiana na uraia wake.Uchunguzi utakapokamilika, matokeo ya uchunguzi huo yatatolewa,"amesema Kamishna Kihinga.

Amefafanua ieleweke kuwa uchunguzi wa utata wa uraia umekuwa ukifanyika kwa watu mbalimbali wakiwemo watu mashuhuri katika jamii.Hivyo suala hilo limeibua hisia huenda kwa kuwa mhusika ni mwanahabari.

Amesisitiza Idara ya uhamiaji imekuwa ikishirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali , kwa hiyo hilo sio suala geni.

Hata hivyo idara hiyo imetoa mwito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa mbalimbali ya kiuhamiaji ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama.Baada ya taarifa hiyo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania vilitaka kufahamu atashikiliwa kwa muda gani na kwa taarifa za awali Kabendera anahusishwa na uraia wa taifa gani.

Kamishina Kihinga amejibu wataendelea kumshikilia hadi pale watakapokamilisha taarifa wanayoihitaji na kuhusu taifa gani anahusishwa nalo hilo kwa sasa bado kwani ndio wanaendelea kukusanya taarifa.

Alipoulizwa Kabendera amekamatwa na nani? Amejibu amekamatwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi. Alipoulizwa kwanini waliokwenda kumkamata hawakutaka kutoa vitambulisho na walikuwa wamevaa kiraia, amejibu wana mbinu nyingi za kumkamata mtu ambaye ameitwa na kisha akakaidi.Hivyo waliamua kutumia mbinu ya kutovaa sare za uhamiaji.