Rais wa Marekani Donald trump ameendeleza shutuma zake dhidi ya balozi wa Uingereza nchini Washington, Sir Kim Darrach akisema kuwa hatoshirikiana naye tena.

Katika matamshi yake katika mtandao wa Twitter rais Trump pia alimshutumu waziri mkuu wa Uingereza Theresa May akisema kuwa ''ni habari njema kwamba Uingereza itapata waziri mkuu mpya''.

Sir Kim katika barua pepe zilizofichuliwa siku ya Jumapili aliutajaa utawala wa rais Trump kama usiofanya kazi na usiojielewa. Bi May alisema kuwa ana imani na Sir kim lakini hakubaliana naye.


Msemaji wake ametaja ufichuzi huo kama usiokubalika na kusema kuwa afisi ya waziri mkuu imewasiliana na Ikulu ya Whitehouse.

Bwana Trump tayari alikuwa amejibu barua hizo zilizofichuliwa kwa kusema 'hatumpendi yule jamaa na hajaifanyia kazi Uingereza vizuri'.

Katika msururu wa machapisho yake ya Twitter alisema kua bwana Kim hakupendelewa sana mjini Washington.

Na baada ya kukasirishwa na hatua ya bi May kumuunga mkono balozi huyo alibadilisha shutuma zake na kuanza kusema vile bi May alivyoshindwa kusimamia Brexit.

Bi May alijiuzulu baada ya kukosa kuungwa na bunge kuhusu mpango wake wa Brexit na chama tawala kinachagua kati ya mgombea Boris Johnson au Jeremy Hunt - kuchukua wadhfa wake.

Idara ya maswala ya kigeni ya Marekani ilikataa kutoa tamko lolote kuhusu matamshi hayo ya Trump

Je balozi huyo sasa hawezi kuruhusiwa kuingia Marekani?

Kwa kusema kwamba hatoshirikiana naye Sir Kim Darroch , Donald Trump anamaanisha kwamba balozi huyo hatakiwi nchini mwake, hiyo ndio njia rasmi ambapo serikali humtimua mwanadiplomasia wa kigeni.

Swala kuu sasa ni nini haswa rais huyo alichomaanisha kuhusu neno 'kuhusiana'.

Iwapo bwana Trump anamaanisha kwamba utawala wake wote hautashirikiana naye basi serikali ya Uingereza italazimika kuamua kumuondoa mjumbe wao mjini Washington.

Sir Kim mbaye ni mtu muheshimiwa na ambaye alitarajiwa kujiuzulu hivi karibuni huenda akaamua kujiuzulu.

Hatahivyo iwapo bwana Trump anamaanisha kwamba hatoshirikiana na Sir Kim basi balozi huyo huenda akasalia hadi pale waziri mkuu atakapofanya uteuzi wake.

Hii inamaanisha kwamba taifa la Uingereza litawekwa katika hali ya sitofahamu ya kukubali shinikizo ya Marekani na kumrudisha nyumbani bwana Kim - hatua itakayoifanya kuonekana dhoofu ama kuwa na msimamo na kumtetea balozi wake kwa kufanya kazi yake na kusema ukweli hatua ambayo huenda ikahatarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili