Raisi wa Marekani, Donald Trump amesisitiza kuwa yeye si mbaguzi baada ya mashambulizi yake kupitia Twitter dhidi ya wabunge wanne wanawake kukemewa vikali.

Katika ukurasa wa Twitter aliwataka wanawake hao wasio na asili ya Marekani, ''kuondoka'' kuelekea kwenye nchi zao walipotoka.

Kitendo hicho kiliamsha ghadhabu, alikataa shutuma kuwa yeye ni mbaguzi: ''sina asili ya ubaguzi mwilini mwangu!''.

Bunge la wawakilishi linajiandaa kupigia kura makubaliano ya pamoja ya kukemea kauli zake, huku hatua hiyo ikitegemewa kupita kutokana na kuwepo wawakilishi wengi wa Democrats.

Awali, wabunge Alexandria Ocasio-Cortez, Ilhan Omar, Ayanna Pressley na Rashida Tlaib walitangaza kupuuza matamshi ya Trump wakidai yanalenga kuwaondoa kwenye mstari.

Wabunge hao waliwataka watu nchini humo kupuuza maneno yake.


Raisi Trump hakutamka majina ya wanawake hayo kwenye ukurasa wa Twitter, lakini yaliyokuwemo kwenye matamshi yake yalionesha wazi kuwepo kwa uhusiano na wabunge hao.

Alisababisha hasira baada ya kusema wanawake ''ambao asili yao wanatoka kwenye nchi ambazo serikali zake ni zina machafuko'' warejee makwao.

Wakizungumza na waandishi wa habari wanawake hao wamesema, hivi sasa watu waweke akili zao kwenye sera za nchini Marekani na si maneno ya raisi Trump.