*Washindi waishukuru Serikali kwa kuwashika mkono na kuishauri jamii kutowatenga watu wenye ulemavu

*BASATA yafurahishwa na ushindi, yahaidi ushirikiano zaidi

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
KWA mara ya kwanza Tanzania imeshiriki katika mashindano ya urembo ya kimataifa ya viziwi (Miss Deaf International) na mrembo Winfrida Bryson  kuongoza kwa kushika nafasi ya kwanza katika vipengele vya ubunifu wa mavazi, mitindo na utamaduni katika mashindano hayo ya urembo yaliyofanyika kuanzia Julai 7 hadi 15 mwaka huu huko mjini St.Petersburg nchini Urusi.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea walimbwende hao Naibu Waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo Juliana Shonza amesema kwamba Wizara imefurahishwa na ushindi huo ukizingatia ni mara ya kwanza wanashiriki mashindano ya kimataifa ya aina hiyo na amewapongeza washiriki hao kwa juhudi zao za kuonesha ubunifu na hatimaye kurudi na ushindi nyumbani.

"Tumefurahi kwa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania, Wizara itaendelea kutoa ushirikiano na ninawahimiza wazazi ambao wana watoto wenye matatizo ya ulemavu wawawezeshe watoto na sio kuwafungia ndani, hii ni dalili njema na tunaamini watafika mbali zaidi hasa kama jamii tukionesha ushirikiano kwao" ameeleza Shonza.

Aidha Shonza amewaomba wadau mbalimbali kukitokeza ili kuweza kufadhili shughuli mbalimbali wanazozifanya na hiyo ni sambamba na kuwatumia katika matangazo mbalimbali ya kijamii.

Aidha amesema kuwa wazazi na wanajamii wasiwatenge watoto wenye aina yoyote ya ulemavu bali wawezeshe kile wanachokipenda ili kuleta matokeo yenye tija.

Kwa upande wake Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye walemavu Stella  Ikupa ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwashika mkono watu wenye ulemavu bila kujali tofauti zao na kuwaomba wadau wengi zaidi kujitokeza kushirikiana nao ili kupeleka taifa mbele zaidi.

Ikupa amewashukuru wazazi wa walimbwende hao kwa ushirikino walioonesha na kuwataka wazazi wengine wanaoishi na watoto wenye ulemavu kutowachukulia tofauti na watoto wengine katika malezi.

Pia katibu mtendaji mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza ameeleza kufurahisha na ushindi kutoka kwa walimbwende hao na kuahidi kushirikiana nao katika kila hatua ili kuzidi kupeperusha vyema bendera ya taifa.

"Ushindi huu wa Winfrida na   Grace sio wa kwao pekee bali wameitangaza nchi na limekuwa jambo jema zaidi kwa kuwa ni mara ya Kwanza Tanzania kushiriki katika mashinano hayo, Baraza litaendelea kushirikiana nanyi katika kila hatua" ameeleza Mngereza.

Aidha kituo hicho cha KISUVITA kimeishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii  kwa kugharamia warembo hao na mkuu wa msafara pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Wizara husika chini ya uongozi wa Waziri Dkt. Harrison Mwakyembe na naibu Juliana Shonza.

Katika mashindano hayo Tanzania iliwakilishwa na warembo wawili ambapo Grace Mtui alishiriki mashindano hayo ya Urembo na kuwa kati ya washindi 10 bora huku Winfrida pamoja na ushindi huo pia alishika nafasi ya 10 kwenye mashindano hayo ya Urembo ya Kimataifa ya Viziwi (Miss Deaf International.) Nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mrembo kutoka Botswana, wa pili Kenya na wa tatu Urusi.
 Mkurugenzi mtendaji mkuu wa Baraza la sanaa la taifa (BASATA) Godfrey Mngereza akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwapokea walimbwende hao ambapo ameeleza kufurahishwa na ushindi huo ulioletwa nchini kwa mara ya kwanza na kuahidi kwamba  baraza litaendelea kushirikiana nao ili kupeperusha vyema bendera ya taifa, jijini Dar es Salaam.

 Washindi wa mashindano ya urembo ya kimataifa kwa viziwi Grace Mtui (kulia) na Winifrida Bryson (kushoto) wakiwa na viongozi waliokuja kuwalaki uwanjani hapo katikati ni Mkurugenzi mtendaji mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza walioketi ni naibu Waziri wa Sanaa, habari na michezo Juliana Shonza (kushoto) na naibu waziri...
 Winifrida Bryson ambaye ni mshindi wa kwanza katika vipengele vya ubunifu wa mavazi, mitindo na utamaduni na mshindi wa kumi katika mashindano hayo ya urembo ya kimataifa kwa viziwi (Miss Deaf International) akiwa na viongozi waliokuja kumpokea ambapo kwa kutumia lugha ishara ameeleza kuwa wao kama walemavu wana nafasi ya kuleta mabadiliko katika jamii na amewataka walemavu kushirikiana zaidi, jijini Dar es Salaam.
 Washindi wa Miss Deaf International wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi, ndugu na wanachama wa kituo Cha sanaa na utamaduni kwa viziwi nchini (KISUVITA), jijini Dar es Salaam.
Grace Mtui, mshindi wa kumi bora katika mashindano ya urembo ya  Miss Deaf International akizungumza kwa lugha ishara mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na kueleza kuwa mashindano hayo yamewapa uzoefu wa kutosha na ameishukuru serikali na Wizara inayowasimamia kwa kuwashika mkono jijini Dar es Salaam.