Tangazo la kuwa Nicki Minaj atakuwa mmoja ya wasanii watakaotumbuiza katika tamasha la muziki nchini Saudi Arabia, limezua gumzo kali katika mitandao ya kijamii nchini humo.

Mtindo wake wa mavazi na maudhui ya ngono katika nyimbo zake ni baadhi ya masuala watu wanahoji huku wakitafakari tamasha hilo litapokelewaje katika jamii ya kihafidhina ya Waarabu.

Rappa huyo anatarajiwa kutumbuiza watu katika tamasha la Jeddah World Fest Julai 18.

Tamasha hilo ni mfano wa hivi karibuni wa jinsi Saudi Arabia inavyoendelea kulegeza misimamo yake mikali hasa katika masuala ya burudani ili kuimarisha ukuaji wa sekta ya sanaa.

"Nicki Minaj" alitrend katika mtandao wa Twitter baada tamasha lake la Jeddah kutangazwa.

"Hebu tafakari kupata fahamu baada ya kupoteza fahamu kwa miaka mitatu na ukizinduka kitu cha kwanza unasikia ni kuwa Nicki Minaj atafungua tamasha la muziki Saudi Arabia, kusema kweli nitafikiria niko katika taifa lingine ," mmoja aliandika.

Mwingine alihoji ikiwa waandalizi wa tamasha hilo walifanya ukaguzi wa maonesho yake yaliopita japo angalau katika mtandao wa Google kabla ya kumpa kazi hiyo. "Hivi hakuna mtu Saudi Arabia aliyemtafuta Nicki Minaj kwenye google?" aliandika Kabir Taneja.

Haki miliki ya picha@KABIRTANEJA
Sio maoni yote yalikuwa ya kufanya mzaha. Mtu mmoja aliandika katika Twitter yake kuwa tamasha hilo la Minaj halitakuwa sawa hasa ikizingatiwa kuwa litafanyika karibu na mji Mecca- amabo ni mtakatifu kwa waumini wa Kiislam .

Katika video iliyowekwa kwenye Twitter mwanamke aliyevalia mavazi ya kidini alihoji kwa nini mamlaka ya nchini humo inamrusu rapa huyo kutumbuiza katika tamasha hilo huku ukiwazuia wanawake kuvaa mavazi yanayowabana hadharani.