Taifa Stars imeambulia Sh.1.3Bil kwa kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi lake la Afcon na inatua leo Alhamisi ikitokea Misri.

Stars haikuambulia pointi hata moja katika michuano hiyo baada ya kupokea vipigo katika mechi zote tatu katika hatua ya makundi kwa kuanza mchezo wa kwanza dhidi ya Senegal 2-0, Kenya 3-2 na mchezo wa juzi dhidi ya Algeria 3-0.

Awali kabla ya kikosi hicho kuelekea nchini Misri kocha mkuu, Emannuel Amunike aliita kikosi cha pamoja kitakachoshiriki Afcon na Chan kisha kukichuja ambacho ndicho anachokitarajia kufanya maandalizi ya michuano hiyo.

 Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema kikosi kitaondoka Misri siku ya Jumatano usiku na kufika Dar Alhamisi.

“Kikosi cha timu ya taifa kitarejea nchini Alhamisi na wachezaji watakwenda mapumziko baada ya muda mwalimu atakiita kikosi chake kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Chan ambapo kitaingia katikati ya mwezi huu.

“Matokeo ambayo tuliyoyapata katika michuano hii sio ya kufurahisha hivyo ni muda wa kujipanga kwa ajili ya mashindano yanayofuata na mambo ya kiufundi tunaliachia benchi hilo litafanyia kazi, hivyo kwa kuliona hilo tumeanza kuandaa michuano ya vijana Copa Championi itakayosaidia kuibua vipaji,” alisema Ndimbo.