Kesi ya uhujumu Uchumi namba 36 ya mwaka 2019,  inayomkabili, Shamim Mwasha (41) na Mumewe Abdul Nsembo maarufu kama Abdulkandida (45), leo Julai 8 imepigwa kalenda hadi Julai 22.

Kesi hiyo ya usafirishaji wa madawa ya kulevya imeahirishwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kusubiriwa kielelezo kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Ilifika mahakamani hapo leo Julai 8 kwa lengo la kutajwa. Akizungumza mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Kazi Kisutu, Wakili wa upande wa mashtaka, Wankyo Simon amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni majibu ya kielelezo kutoka kwa Mkemia na kuomba tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa.

Mara baada ya maelezo hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Wakili upande wa utetezi, Hajra Mungula amedai washtakiwa wako ndani na hawana dhamana, na kuutaka upande wa mashtaka kufuatilia kielelezo hicho ili majibu yapatikane.

Shamim na Mumewe wanashtakiwa kwa kosa la usafirishaji wa madawa ya kulevya aina ya heroin kinyume cha sheria, ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 1, 2019 nyumbani kwao maeneo ya Mbezi Beach, ambapo walikutwa na dawa hizo zenye uzito wa gram 232.70.