Katibu Mkuu wa Wizara ra Mifugo na Uvuvi, Dkt. Elisante Ole Gabriel amesema kila Mtanzania anatakiwa kula kilo 50 za nyama kwa mwaka ili kuwafanya wawe na afya bora, pamoja na kuwataka Watanzania kuongeza zaidi suala la ulaji wa nyama.


Katibu Mkuu Elisante Ole Gabriel ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea Makao Makuu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) jijini Dodoma, ambapo amesema kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), kila Mtanzania anakula kilo 15 tu kwa mwaka jambo ambalo si toshelezi.

"Mtazamo wetu kama Wizara, NARCO itumie fursa hii ya ya soko la nyama hapa Tanzania kwa ajili ya kuuza na kuhamasisha watanzania kula nyama, takwimu za Shirika la Chakula Duniani zimeonesha Watanzania wengi ni wavivu kula nyama.", amesema Ole Gabriel.

"Takwimu zinaonesha kila Mtanzania anatakiwa kula nyama kilo 50 kwa mwaka, lakini Watanzania ni wavivu kula nyama ndiyo maana takwimu zinaonesha kila Mtazania anakula kilo 15 kwa mwaka, kwa hiyo muhimu sana NARCO wakatumia fursa hii" ameongeza.